In Summary

Tofauti na siku za nyuma wakati waandaaji walikuwa wakionywa, safari hii hakuna anayeweza kusema maandamano hayo yanaratibiwa wapi, nani anayaandaa, lengo lake nini na yataanzia wapi?

Dar es Salaam. Maandamano! Viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi nchini wamepiga marufuku na kuonya atakayejaribu kuandamana kuchukuliwa hatua kali.

Tofauti na siku za nyuma wakati waandaaji walikuwa wakionywa, safari hii hakuna anayeweza kusema maandamano hayo yanaratibiwa wapi, nani anayaandaa, lengo lake nini na yataanzia wapi?

Vyama vya upinzani, baadhi ya mashirika yasio ya kiserikali na taasisi za kutetea haki za binadamu zimekana kuandaa maandamano yoyote jambo ambalo limezua maswali zaidi kutokana na onyo la Serikali.

Makamanda wa polisi wa baadhi ya mikoa wamesema hakuna maombi yoyote waliyoyapokea kuhusu maandamano hayo.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wamesema kuwa kitendo cha viongozi wa Serikali na Polisi kuzungumzia maandamano hayo ni sawa na kupambana na kitu ambacho hakionekani kwa sababu ndani ya mipaka ya Tanzania hakuna aliyekiri kuandaa maandamano.

Si Chadema, CUF, ACT-Wazalendo au NCCR-Mageuzi walioyaandaa; si Jukwaa la Katiba Tanzania au Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wanayoyatambua.

Wakati vyama na asasi hizo za kiraia zikikana kuyatambua, baadhi ya makamanda wa Polisi wa mikoa wamelieleza Mwananchi kwamba hakuna barua zozote zilizofika vituoni kuomba maandamano.

“Wakati tunahangaika kuiletea nchi maendeleo, wapo watu wanapanga kuandamana...waandamane niwaone. Wataenda kuwahadithia baba zao,” alisema Rais John Magufuli Machi 9, akizindua jengo jipya la CRBD mjini Chato mkoani Geita.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba akiwa mjini Singida juzi alizungumzia maandamano hayo akisema kasi anayoifanya Rais Magufuli katika utekelezaji wa maendeleo ndiyo imekuwa ikiwasumbua wapinzani na wasijue la kufanya.

“Kinachotafutwa si kuwa na mabango, kinachotafutwa ni watu kukusanyika na ikitokea namna yoyote ya kutawanya watu, wafyatue risasi ili waseme Serikali imeua watu na njama hiyo tumeiona,” alisema Dk Nchemba.

Alisema, “Nimemwelekeza IGP kwamba hata kupanga njama ya kuua ni kosa, wachukue hatua kwa wale wanaopanga njama hizo na kuchafua taswira ya nchi.”

Katika kusisitiza hilo, Dk Nchemba alisema, “Hakuna sababu ya maandamano, wala hakuna sababu ya kuandamana na hakuna ruhusa ya kuandamana. Na ikatokea hata watu wakaandamana ndani ya nyumba kuzunguka kitanda, ikatokea mtu akaumia, yule aliyewaita wakaandamana atawajibika.”

Mwananchi lilizungumza na makamanda wa Polisi, Jaffari Mohammed (Mara), Mohamed Mpinga (Mbeya), Juma Bwire (Iringa) na Kaimu Kamanda wa Polisi Arusha, Yusuph Ilembo ambao kwa nyakati tofauti walisema hawajapokea maombi yoyote ya kufanyika kwa maandamano.

Mbowe, Zitto wahoji

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipoulizwa na Mwananchi kama wameandaa maandamano alicheka na kusema, “Waulizeni hao wanaotoa hizo kauli ni ya nani, wanapambana na hewa?”

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alihoji akisema, “Watangaze na kusema hayo maandamano ni ya nani, sisi hatujatoa kauli au kuandaa maandamano, waseme ni maandamano ya nani.”

Kauli ya Mbowe ni sawa na ya Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyesema, “Nami nasikia habari za maandamano kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.”

Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini alisema, “Ninachojua ni kuwa maandamano ni ya wananchi, haki ya kikatiba. Sisi ACT-Wazalendo hatujaandaa maandamano, lakini iwapo wananchi wataamua kutumia uhuru wao wa Kikatiba kuandamana tutawaunga mkono kwa kuwa ni haki yao Kikatiba.”

Abdul Kambaya, mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa CUF, upande wa Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, alisema hawatambui na wala chama hicho hakijawahi kukaa vikao vya kuratibu maandamano.

“Maandamano ni hatua ya mwisho ya kushinikiza jambo kama hakuna maridhiano, sisi upande wetu hakuna kitu kama hicho kwa sababu hakuna kikao chochote kilichoketi kujadili suala hilo,” alisema Kambaya.

Majibu ya Kambaya yanaungwa mkono na katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju aliyekana chama hicho kuandaa maandamano au kuyafahamu.

Alisema hawajawahi kukaa vikao vyovyote kama chama au wakiwa chini ya mwavuli wa vyama vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, CUF na Chadema kujadili suala la maandamano yanayopigwa marufuku. “Hatutambui na wala hatujui suala linalohusu maandamano, hatutambui kama taasisi na hata tukiwa chini ya mwavuli wa Ukawa. Umoja wetu haujakaa kujadili suala lolote kuhusu maandamano,” alisema.

Juju alisema, “Kwa hiyo nasema kama mtendaji wa taasisi yangu, jambo hilo halipo.”

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema, “Hatujaandaa maandamano yoyote labda wao wamtaje aliyeandaa na kama ni chama akitaje, tunachojua ni maandamano yanayoratibiwa na wananchi wenyewe.”

Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Hebron Mwakagenda licha ya kutotaka kuzungumzia maandamano yanayozungumzwa alisema wanaoyaandaa wana haki Kikatiba, hivyo waruhusiwe.

Hata hivyo, alisema wao kama Jukata wana maandamano ambayo wameyakatia rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba.

“Hatuwezi kuzungumzia maandamano ya Aprili 26, lakini wanayoyaandaa wana haki kikatiba kwa hiyo waruhusiwe. Maandamano hayo yana madai ya haki na sisi tutakuwa sehemu yake tu maana tuna madai yanayofanana,” alisema Mwakagenda.

Akizungumzia maandamano yao, alisema walishaomba kibali kwa Jeshi la Polisi wakanyimwa na sasa wamekata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

“Sheria inatutaka tufuate utaratibu huo, tumeomba kibali Polisi tumekataliwa sasa tuko kwa waziri. Itategemea jibu atakalotupa, lakini akitukatalia tunakwenda mahakamani, tutapata haki yetu maana unapokwenda mahakamani umejiandaa kushinda,” alisema.

Inadaiwa kuwa maandamano ambayo yamekuwa yakitajwa yanaandaliwa kwenye mitandao ya kijamii huku ikidaiwa kuwa wengine wamepanga kuandamana nje ya nchi Aprili 25.