In Summary

Katibu Mkuu wa CUF,  Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jeshi la Polisi kisiwani Pemba limefanya kazi kwa weledi katika kipindi chote cha ziara yake ya siku nne kisiwani humo


Pemba. Katibu Mkuu wa CUF,  Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jeshi la Polisi kisiwani Pemba limefanya kazi kwa weledi katika kipindi chote cha ziara yake ya siku nne kisiwani humo.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 11, 2019 mara baada ya kumaliza ziara yake hiyo ambako alitembelea wilaya zote nne za Pemba.

Amesema katika kipindi chote akiwa Pemba kulikuwa na usalama na kwamba huenda bila uwepo wa askari polisi kungeweza kujitokeza viashiria vya uvunjifu wa amani.

Amesema ipo haja ya polisi kuchukulia ziara hiyo kuwa  mfano wa kuigwa katika kipindi chote cha utendaji wao wa kazi.

“Ufanyaji huu wa kazi ukiendelea  hakuna mwananchi wala kiongozi wa chama cha siasa atakayelilalamikia jeshi hili,”amesema Maalim Seif.

Kiongozi huyo amewataka watendaji wa polisi kutokubali kutumiwa na viongozi wa Serikali au vyama vya siasa badala yake kufanya kazi kwa misingi ya miongozo yao inavyowaelekeza.

Maalim Seif na ujumbe wake wamemaliza ziara ya siku nne kisiwani Pemba leo na kurejea Unguja.