In Summary
  • Baraza la habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa pamoja wamelaani kitendo cha kukamatwa maofisa wa Kamati ya Ulinzi wa Waandishi wa Habari (CPJ) kwa madai kuwa utaratibu uliotumika hakuwa mzuri na unachafua sifa ya amani ya nchi.

Des Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa pamoja wamelaani kitendo cha kukamatwa kwa waandishi wawili wa Kamati Maalum ya Ulinzi wa Waandishi wa Habari (CPJ).

 

Waandishi hao ambao ni Angela Quintal raia wa Afrika Kusini na Muthoki Mumo raia wa Kenya walikamatwa na maofisa wa Idara ya Uhamiaji jzui Novemba 7, 2018 katika Hoteli ya Southern Sun iliyopo jijini hapa kwa madai kuwa walikiuka maelezo ya vibali vyao vya kuingia nchini.

"Maofisa hao walikuja kuwatembelea wana tasnia wenzao, walipokamatwa hawakuelezwa kosa lao na kama walikuwa wamefanya makosa kulikuwa na njia nyingine nzuri ya kuwakamata kuliko iliyotumika kwa kuwakamata usiku kwani wangeweza kusubiri asubuhi," amesema Kaimu Katibu Mtendaji wa MCT, Pili Mtambalike.

 

Mratibu wa Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumo amesema kibali cha maofisa hao waliorejea katika nchi zao siku moja baada ya kukamatwa, kilieleza kuwa wamekuja kwa ajili ya kuwatembelea wenzao katika tasnia hivyo kufanya mahojiano na mikutano pamoja nao si kinyume cha kibali.

"Niombe vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya kazi kwa weledi kwa kuheshimu sheria za nchi na mikataba ya kimataifa ambayo nchi imeridhia lakini pia waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu wote waamke wapaze sauti ili matukio kama haya yasijirudie," amesema Olengurumo.