In Summary

Msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu ‘Lulu’ amesema alipokuwa gerezani, alipenda kusoma gazeti la Mwananchi alilokuwa akiletewa na ndugu zake

Dar es Salaam. Msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu ‘Lulu’ amesema alipokuwa gerezani, gazeti alilopenda kulisoma lilikuwa ni Mwananchi.

Lulu ameyasema hayo leo Jumatatu Februari 11, 2019 alipotembelea ofisi za Mwananchi zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Msanii huyo ambaye alianza kuigiza akiwa na miaka mitano katika kundi la kuigiza la Kaole, amesema magazeti hayo alikuwa akiyapata wakati ndugu zake wakiwa wanaenda kumtembelea.

“Kule gerezani tunaruhusiwa kuletewa magazeti, hivyo katika ya magazeti ambayo nilikuwa nayapenda Mwananchi ni mojawapo kwani nilikuwa lazima kila siku nilisome.

“Na kati ya habari ambazo zilikuwa zikinivutia zaidi ni zile za simulizi zinazoelezea masuala ya kijamii, mfano yule mama aliyemwagiwa tindikali na mumewe, niliisoma ile habari mwanzo mwisho,”amesema Lulu.

Hata hivyo amesema kuwa kwake gerezani kumemfanya kupenda kusoma habari zilizoandikwa kwa urefu jambo ambalo awali alikuwa hawezi.

Alibainisha kuwa hata ujumbe mfupi kwenye simu mtu kama alikuwa akimtumia mrefu alikuwa anaachana nao lakini sasa hivi hilo analiweza na pia limemfanya awe mpenzi mkubwa wa kusoma vitabu.

Novemba 13, 2017  Lulu alihukumiwa kwenda jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia, aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Hata hivyo Mei mwaka jana alibadilishiwa adhabu hiyo na kuwa kifungo cha nje, adhabu ambayo alimaliza kuitumika Nevemba 12, 2018.