In Summary

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema mkazi yeyote asinunue ardhi bila kuonana na wataalamu wa Manispaa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na wala asimwamini hata Kiongozi wa serikali za mitaa.

Dar es salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema mkazi yeyote atakayenunua ardhi bila kuonana na wataalamu wa Manispaa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ajiandae kununua ‘bomu’.

Amesema yeyote atakayekaidi agizo hilo na akatapeliwa, hatapatiwa msaada kutoka serikalini.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumatatu Aprili 15, 2019 alipokuwa akizungumza na wakazi wa Vijibweni, Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya mkutano wa kushughulikia mgogoro kati ya Mwekezaji na wakazi wa Vijibweni, uliodumu tangu 2004.

Licha ya kushindwa kesi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi mwaka 2018, wakazi 124 wa Kata hiyo wenye madai tofauti, wameendelea kudai fidia ya Sh1 milioni kwa hekari moja tofauti na fidia ya Sh400,000 aliyokuwa akiitoa Mwekezaji Mkorea.

Mwekezaji huyo alinunua hekari 305 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu.

Lukuvi amesema wakazi katika mikoa hiyo wasithubutu kuamini hata viongozi wa serikali za mitaa katika maeneo wanayotaka kununua ardhi.

"Kuna mahali nimeshuhudia mwenyekiti wa serikali anagonga muhuri mitatu kwenye kiwanja kimoja na wengine wameanza kutengeneza hati, wanaziita hati za ardhi za mitaa ni marufuku serikali ya mtaa kuwa na hati, hamruhusiwi kisheria," amesema Waziri Lukuvi.