In Summary

Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likitangaza kumfungia Wakili Revocatus Kuuli kifungo cha maisha kutojihusisha na mpira wa miguu, mwenyewe ameibuka na kutamba hababaishwi na uamuzi huo.


Dar es Salaam. Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likitangaza kumfungia Wakili Revocatus Kuuli kifungo cha maisha kutojihusisha na mpira wa miguu, mwenyewe ameibuka na kutamba hababaishwi na uamuzi huo.

Kuuli alikutana na rungu hilo jana, baada ya Kamati ya Maadili ya TFF kutangaza kumpa adhabu ya kutojihusisha na soka maisha yake yote akituhumiwa kuhusika na makosa matatu ya kimaadili.

Makosa ambayo Kuuli alituhumiwa kujihusisha nayo kwa mujibu wa barua ya wito aliyopewa na Kamati ya maadili ya TFF yalikuwa ni kusambaza nyaraka/barua za TFF kinyume na kifungu cha 16(1)na (2) cha kanuni za maadili za TFF toleo la 2013 na kinyume na Ibara ya 12(1)(b).

Mengine yalikuwa ni kutoa maelezo yanayoonyesha kuwa na mgongano wa maslahi kwa kuwapa watu wasiohusika kinyume na kifungu cha 19(2) cha kanuni za maadili za TFF na kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho kinyume na Ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF.

Kikao cha Kamati ya Maadili ya TFF kilichokutana Novemba 3, Dar es Salaam ambacho Kuuli hakuhudhuria, chini ya Mwenyekiti wake Wakili Hamidu Mbwezeleni, ilitoa adhabu ya maisha ya kutojihusisha na soka.

“Uamuzi huu umechukuliwa kwa kufuata kanuni na taratibu. Hakuna aliyemuonea Kuuli niliweke hilo sawa,” alisema Mbwezeleni akitangaza uamuzi huo.

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya adhabu hiyo, Kuuli alisema hataumiza kichwa na uamuzi wa TFF na amejifananisha na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela.

“Kunifungia mimi maisha? Mbona jambo dogo sana kwangu. Nilidhani watanifungia hadi kutazama mpira, kumbe kujihusisha na masuala ya mpira?

“Alifungwa maisha Mandela tena gerezani na akaachiwa huru baada ya miaka 25 na baadaye akawa rais wa Afrika Kusini, sembuse mimi ambaye wamenifungia mambo ya mpira lakini naendelea kudunda mtaani? alihoji Kuuli.

Kuuli alidai waliomfungia maisha ni waoga na alisisitiza adhabu hiyo siyo kubwa kwake kwa kuwa watu wenye busara wanafahamu utendaji wake katika soka.

“Nazifahamu sanaa za pale TFF, lakini hao waliochukua uamuzi huo kwanza niwaambie tu kwamba ni wa kawaida mno kwangu. Kifupi sijashtushwa nao hata kidogo. Ningepata hofu kama wangenifungia kutazama mpira,” alisema Kuuli.

Kuuli aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi iliyoongoza uchaguzi uliomueka madarakani rais wa TFF Wallace Karia, alisema hana mpango wala nia yoyote ya kuwania uongozi ndani au nje ya shirikisho hilo.

“Niwatoe tu wasiwasi kama walidhani nina mpango wa kugombea urais wa TFF basi wakae wakitambua sina fikra hizo wala sijawahi kufikiria,” alisisitiza Kuuli.

Kuuli alisema uamuzi uliotolewa juu yake ni uoga na anachukulia uamuzi wa kufungiwa ni ukosefu wa busara kwa kuwa kila mtu mwenye akili timamu anafahamu haukuwa sahihi.

Uamuzi huo umemshitua aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu, Idd Kipingu alisema ingekuwa vyema TFF ingempa onyo Kuuli kama alitenda makosa hayo kabla ya kufikia hatua ya kumuondoa kwenye familia ya soka.

“Sijui ni kosa lake la ngapi ametenda, lakini kama ni mara ya kwanza ingekuwa vyema kama ingempa tu onyo, lakini sio kumfungia maisha,” alisema Kipingu.

Dalili za kufungiwa Kuuli zilianza baada ya kutangaza kusimamisha kwa muda uchaguzi wa klabu ya Simba, Septemba baada ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF kukutana Dodoma.

Septemba 17, Kuuli alitangaza kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa Simba kwa madai ya kutofuatwa kwa baadhi ya utaratibu na kanuni za uchaguzi.

Hata hivyo siku chache baadaye Sekretarieti ya TFF chini ya Katibu Mkuu Wilfred Kidao ilimuandikia barua Kuuli ikimtaka aipe ufafanuzi wa tamko alilotoa kinyume na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyokutana Dodoma.

Barua hiyo iliyoandikwa na Sekretarieti ya TFF kwenda kwa Kuuli, ilivuja katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii jambo lililosababisha kamati ya maadili kumuita ili kumuhoji akituhumiwa kukosa maadili kwa kuvujisha taarifa hiyo.

Barua hiyo yenye kumbukumbu namba tff/ADM/LM791/2018 ya Oktoba 29, ilimtaka Kuuli ahudhurie au kutuma mwakilishi wake kwenye kikao cha Novemba 3 ambacho hata hivyo hakuhudhuria wala kutuma mwakilishi kama alivyotakiwa na kamati hiyo ambayo ilifikia uamuzi wa kumfungia.

Kuuli anakuwa kiongozi wa tatu kufungiwa maisha chini ya uongozi wa Karia, wengine ni Michael Wambura na Mbasha Matutu.

Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeitaka Klabu ya Yanga kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi za uongozi ikiwemo ya mwenyekiti ifikapo Januari 13, mwakani.