In Summary
  • Vituo vya Magic FM na Radio Free Africa vimepewa onyo kali baada ya kutangaza kwa kina habari za magazeti badala ya vichwa vya habari.  

Dar es Salaam. Kamati ya Maudhui, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa onyo kali kwa vituo viwili vya radio Magic FM na Radio Free Africa kwa kukiuka agizo la Serikali kwa makusudi na kusoma habari magazetini kwa undani badala ya vichwa vya habari.

Uamuzi wa kamati umefikiwa leo Jumatatu, Aprili 15,2019  baada ya pande zote mbili kuwasilisha utetezi wao mbele ya wajumbe baada ya kukikuka agizo la serikali kwa makusudi ambalo lilipitisha mwaka 2017.

Akisoma hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Valeriani Msoka amesema katika muda tofauti Januari 2019, kituo cha Magic FM kupitia programu ya Morning Magic kilisoma habari kwenye magazeti mbalimbali badala ya vichwa vya habari pekee.

Aidha, Radio Free Afrika Januari 2019 mtangazaji alisoma habari kwenye magazeti kwa kina badala ya vichwa habari jambo ambalo linakiuka maelekezo ya Serikali ambayo yanalenga kufanya kampuni za magazeti ziweze kufanya biashara.

“Kamati haikuridhishwa na utetezi kutoka pande zote mbili kwa sababu zao hazikuwa na mashiko, kwa hiyo tunawapa onyo kali kutorudia makosa hayo tena,” amesema Msoka

Msoka ameongeza kamati imetoa mapendekezo kwa vituo vyote viwili ikiwemo kufanya matayarisho ya kutosha kabla ya kipindi kuanza na kuimarisha na kuboresha usimamizi wa vipindi.

Pia watoe mafunzo ya awali kwa watangazaji wao wapya ili wajue taratibu za serikali kwenye kipengele cha magazeti