In Summary

Katika mfululizo wa makala zetu za matumizi ya mkaa na kuni na athari zake, leo tunaendelea kuangalia jinsi Wilaya ya Handeni ilivyoamua kutumia kilimo cha muhogo kama njia ya kuwapa wananchi ajira mbadala ili wasijikite katika uuzaji mkaa.

Handeni. Wafanyabiashara wa mkaa wilayani Handeni mkoani Tanga wamesema serikali imechelewa kuhimiza wananchi katika suala la kupanda ili kulinda uoto wa asili kutokana na maeneo mengi kuathirika baada ya miti kukatwa kwa ajili ya kupata mkaa na mbao.

Wakiongea na Mwananchi kwa nyakati tofauti walisema kwa sasa Serikali inatakiwa kusimamia na kuhimiza upandaji miti kwa wingi kwa kuwa tayari kuna maeneo ambayo mazingira yake yameshaathirika kutokana na kukatwa miti.

Mmoja wa wauza mkaa wa Mtaa wa Zizini, Suphian Rashid anasema maeneo kama Kijiji cha Kwankonje kilichoko Kata ya Kwamsisi mpaka Kwasunga, misitu yake imeharibiwa na wananchi ambao wanazalisha mbao na mkaa.

“Ushauri wangu kwa serikali kama inawezekana tuandae misitu maeneo mbalimbali na isimamiwe kama hizi hifadhi. Ipandwe miti kwa ajili ya kuvuna mbao, mkaa na mazao mengine ya misitu. Hili linawezekana kama kule Mufindi hii ndio itasaidia kupunguza uvunaji misitu hovyo,” anasema Suphian.

Ushauri huo unatofautiana na wa Zuhura Mhando anayeuza mkaa maeneo ya Chanika.

“Kama Serikali inataka kulinda misitu, basi waweke mkakati ili gesi ipungue bei, wananchi waone kutumia mkaa ni gharama kuliko gesi”, anasema Mhando.

Anasema mkaa ni biashara endelevu kwao kwa kuwa una wateja wengi kutokana na ukweli kwamba mtu wa hali ya chini na mwenye uwezo wote wanatumia mkaa.

Alisema wananchi wa hali ya chini ndio watejwa wakubwa wa mkaa na wanauziwa ndoo ndogo (kisado) kwa Sh500 mpaka Sh1,000. Anasema gunia huuzwa kuanzia Sh15,000 mpaka Sh18,00 kwa mwenye uwezo.

“Sisi wengine hatuwezi kutumia nishati ya gesi ambao mtungi wa kilo sita unajazwa kwa Sh22,000 mpaka Sh23,000 kutokana na ulipo. Gharama hiyo tunaona ni kubwa, bora nitumie mkaa,” anasema Mhando.

Muhogo kuokoa misitu

Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe anasema kuwa wameshatoa elimu kwa wadau wa misitu na zaidi ya watumiaji 300 wa mazao ya misitu kuhusu umuhimu wa kukata na kupanda miti ili kunusuru uharibifu wa mazingira.

Anasema kwa kutumia Mfuko wa Misitu Tanzania Wilaya imepatia Sh90 milioni kwa ajili ya shughuli za upandaji miti hivyo wameanzisha kampeni maalumu ya kupanda miti yenye ujumbe “Miti Yangu, Maisha Yangu” inayolenga kuhakikisha miti 5,000 inapandwa.

Gondwe anasema Handeni imefanikiwa kuanzisha mashamba kadhaa ya miti katika maeneo ya barabara iendayo Korogwe kwa lengo la kutoa elimu kwa vitendo kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupanda miti kwenye maeneo yao bila kutegemea miti iliyopo kwenye misitu ya asili.

“Wadau wetu wanaotumia misitu katika Wilaya ya Handeni walikuwa hawana elimu yoyote kuhusu umuhimu wa kukata mkaa, kuvuna mbao na kupanda kupanda miti. Kati ya watu 300 waliohudhuria, saba tu ndio wamepanda miti,” anasema Gondwe.

Anasema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwatoa wananchi wa Handeni katika hali ya kutegemea mazao ya misitu kama mbao na mkaa. Kulima muhogo kumesababisha wananchi kuacha kukata mkaa.

Anasema wapo kwenye utaratibu wa kufuatilia kujua ni watu wananchi wangapi walikuwa wakitegemea mkaa kama biashara yao ya kuendesha maisha, lakini kwa sasa wameacha na kujikita kwenye kilimo cha muhogo.

Biashara ya mkaa yapungua

Pamoja na kilimo cha muhogo, ofisa misitu wa wilaya kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Antony Mwilenga anasema biashara ya mkaa kwa sasa imepungua kwa kuwa awali walikuwa wanakamata mpaka magunia 1,000 ya mkaa kwa mwezi mmoja lakini sasa ni magunia 500 hadi 600 tu.

Anasema idadi hiyo imepungua kutokana na elimu wanayoendelea kutoa kwa watumiaji wa misitu kuhusu umuhimu wa kuitunza kila siku kwenye majukumu yao ya kazi na kwamba wananchi wanaonekana kuelewa.

Anasema ni vigumu kuzuia biashara ya mkaa kwa kuwa wauzaji wengine wanavuna kutoka kwenye mashamba yao. Kwa hao, anasema kinachotakiwa ni kuwahimiza kufuata sheria za uvunaji ili wasisababishe uharibifu wa mazingira.

Anasema kila mwananchi ambaye anavuna mazao ya misitu, lazima afuate taratibu za muongozo wa uvunaji wa misitu wa mwaka 2017 ambao umeeleza mambo yote yanahusu uvunaji.

Miongoni mwa yaliyosisitizwa kwenye muongozo huo ni ulipaji ushuru kwa Serikali pamoja na halmashauri kwenye eneo husika.