In Summary

Wagombea 26 wajitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kinyang’anyiro cha urais DRC

Kinshasa, DRC. Kukubali kung’atuka kwa Rais Joseph Kabila ni ishara nzuri, lakini bado ni mapema kufurahia uchaguzi huru na wa haki katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Kabila ni mwanasiasa wa DRC aliyeiongoza nchi hiyo tangu Januari 2001. Alitwaa madaraka siku kumi baada ya kuuawa kwa baba yake, Laurent Desire Kabila aliyekuwa rais wa nchi hiyo.

Juzi, kiongozi huyo alivunja ukimya kwa kumtangaza waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Shadary kuwania urais kupitia muungano wa vyama tawala wa Common Front for Congo (CFC).

Shadary aliwasilisha fomu zake za kuwania urais kwa Tume ya Uchaguzi juzi mchana saa chache kabla ya muda uliowekwa kuchukua na kurejesha kukamilika.

Uchaguzi Mkuu nchini humo unatarajiwa kufanyika Desemba 23, baada ya kuahirishwa kwa muda mrefu na kusababisha vifo vya watu kadhaa wakiwa wanaandamana kumpinga Kabila kuwania tena urais.

Kwa mujibu wa katiba ya DRC, Kabila hakupaswa kuwania muhula mwingine, lakini hilo halingemzuia kuahirisha uchaguzi huo ambao umekuwa ukibadilishwa kalenda tangu mwaka 2016.

Kumekuwapo na shinikizo kubwa kutoka jumuiya ya kimataifa na mashirika ya kiraia nchini humo kama vile Lucha na makundi ya kanisa yanayompinga Kabila kuwania muhula wa tatu.

Licha ya kuchelewa, lakini uamuzi wa kiongozi huyo ni ishara chanya hata kwa mataifa jirani. Ishara ya matumaini kwamba inawezekana kuzuia utawala wa maisha kwa njia za amani.

Hata hivyo, bado ni mapema kujua kama mgombea huyo ana ajenda yake mwenyewe ya mageuzi kwa ajili ya Taifa hilo lenye mikoa 26 ambalo ukubwa wake unazidi kanda nzima ya Ulaya ya Kati.

Tayari fununu zimeanza kuzagaa kwamba Shadary ni rafiki mkubwa wa Kabila ambaye ataendeleza sera zake na pia taasisi zote za kiserikali zipo kwa ajili yake na huenda hilo likawa jambo litakalomsaidia kutumia rasilimali za Serikali wakati wa kampeni za uchaguzi.

Ikiwa uchaguzi utafanyika Desemba 23, 2018 kama ilivyopangwa, kinyang’anyiro kinatarajiwa kuwa cha kukata na shoka kati ya Shadary na Jean-Pierre Bemba atakayepeperusha bendera ya chama cha upinzani cha MLC. Yeyote atakayeshinda kati yao atakabiliwa na changamoto nyingi kubwa.

Pia katika miaka ya utawala wa Kabila kumekuwapo na ongezeko la wakimbizi waliokwenda nchi za jirani na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu vikiambatana na rushwa iliyokithiri, upendeleo, viwango vya juu vya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na umaskini uliopindukia.

Wananchi wa Kongo hawajui kinachoitwa uchaguzi huru na wa haki mpaka sasa tangu walipopata uhuru. Lingekuwa jambo jema wananchi wakayaona mabadiliko chanya na kwa rais ajaye kufanya kazi kwa manufaa ya raia na mustakabali wa Taifa.

Shadary amesema akichaguliwa atahakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa amani na hali yao ya maisha itakuwa bora.

Ferdinand Kambere, naibu katibu mtendaji wa chama tawala cha PPRD, anasema kwamba uteuzi wa Shadary ni alama ya ushujaa wa demokrasia nchini humo.

Nguvu ya upinzani

Kwa upande mwingine, upinzani umeelezea kwamba uteuzi wa mgombea wa chama tawala ni hatua ya ushindi wa demokrasia kwa kuwa Kabila hagombei, lakini wanatarajia uchaguzi huru na wa haki. Martin Fayulu ambaye ni mgombea wa vuguvugu Dynamique de l’opposition anasema raia ndio wanaotakiwa kuamua kupitia uchaguzi na si vyombo vya Serikali.

Anasema hawana maoni yoyote juu ya mteule huyo anayetarajiwa kumrithi Kabila na kwamba, ni mambo yao ya ndani.

Anasema ikiwa Rais Kabila amepanga njama ya kurejea madarakani baadaye kama walivyofanya Rais Vladimir Putin wa Russia na rafikiye Dmitry Medvedev, hiyo ni haki yake, lakini akaonya kwamba wanachotaka ni uwepo wa uchaguzi huru, wa wazi na wa kidemokrasia ili kuruhusu raia kujichagulia viongozi wao.

Miongoni mwa wagombea wane wa upinzani ni pamoja na Jean Pierre Bemba, Vital Kamerhe na Felix Tshisekedi ambaye ni kiongozi wa chama cha UDPS.

Wagombea watatu ni wanawake ambao wawili wameishi ugenini akiwemo Monique Mukuna. Pia yumo Waziri Mkuu wa zamani na mshirika wa Rais Kabila, Antoine Gizenga (94).

Bado kuna tetesi kwamba upinzani nchini humo umepungua nguvu ikilinganishwa na awali na hii inatajwa kuwa sababu iliyomfanya Kabila kuachia madaraka kirahisi.

Bemba ambaye aliachiwa huru na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC), kwa kufutiwa makosa yote aliyokuwa anakabiliwa nayo ya uhalifu uliotokea katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kati ya mwaka 2002 na 2003, inadaiwa kwamba hana wafusi wengi kama ilivyokuwa awali.

Mgombea mwingine wa upinzani anayetajwa kwamba hana wafuasi wengi ni Felix Tshisekedi, kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS). Felic ni mtoto wa mwanasiasa maarufu nchini humo, Étienne Tshisekedi aliyefariki dunia mwanzoni mwa mwaka jana.

Pia yupo mgombea huru, Tryphon Kin-Kiey Mulumba aliyewahi pia kuwa waziri katika Serikali ya Kabila.

Nguvu ya upinzani imezidi kuporomoka baada Serikali kumzuia mfanyabiashara maarufu Moise Katumbi (53), kuingia nchini humo.

Mfanyabiashara huyo tajiri na gavana wa zamani wa Mkoa wa Katanga hakuwasilisha fomu zake za kuwania urais.

Katumbi amekuwa akiishi nchini Ubelgiji tangu Mei, 2016 baada ya kutofautiana na Rais Kabila.