In Summary

Carlos Ghosn ameachiwa huru kwa dhamana baada ya kukamatwa na kukaa mahabusu kwa zaidi ya siku 100 kutokana na makosa ya ufisadi.

Tokyo. Mahakama nchini Japan leo Jumatatu imemzuia Carlos Ghosn kuhudhuria kikao cha bodi ya kampuni ya Nissan, wakati mwenyekiti huyo aliye nje kwa dhamana akijiandaa kujibu mashtaka dhidi ya ukiukwaji wa taratibu za fedha.
Nissan ilimuondoa Ghosn katika nafasi yake baada ya kukamatwa mwezi Novemba, lakini haiwezi kumvua rasmi uenyekiti wa bodi kabla ya kuitishwa kwa mkutano maalum wa wanahisa ambao unatarajiwa kufanyika Aprili 8.
"Ghosn aliomba kuhudhuria mkutano wa bodi lakini mahakama haikuidhinisha kuhudhuria kwake," mahakama ya wilaya ya Tokyo ilisema katika taarifa yake.
Bodi ya kampuni hiyo ya kutengeneza magari ya Japan inakutana kesho mjini Yokohama, karibu na Tokyo.
Na mwanasheria wa Ghosn anayeitwa Junichiro Hironaka alisema mapema leo kuwa mteja wake alikuwa na "jukumu" la kuhudhuria kikao cha bodi na alitaka kufanya hivyo kama mahakama ingemruhusu.
Katika kauli aliyoitoa baadaye kwa waandishi, Hironaka alisema Nissan iliwasilisha maoni yake kimaandishi kwa waendesha mashtaka ikiomba Ghosn azuiwe kuhudhuria kikao cha bodi.
Mwanasheria huyo aliongeza kuwa anafikiria kukata rufaa kupinga zuio la mahakama.
"Hatukutegemea (Nissan) ipinge kwa nguvu namna hiyo," alisema Hironaka.
Ghosn aliachiwa kwa dhamana ya karibu dola 9 milioni za Kimarekani Machi 6.
Chini ya masharti yaliyo katika dhamana yake, amezuiwa kuwasiliana na watu ambao wanaweza kuhusishwa katika kesi hiyo, wakiwemo watendaji wa Nissan ambao wanaweza kuhudhuria kikao cha bodi, kama vile ofisa mtendaji mkuu wa Nissan, Hiroto Saikawa.
Masharti mengine ya dhamana yake ni pamoja na kufuatiliwa kwa kamera zilizofungwa nje ya nyumba yake. Anaweza tu kutumia kompyuta ambayo haijaunganishwa na internet na ataitumia kwenye ofisi ya mwanasheria wake.
Tajiri huyo wa zamani wa magari alitoka nje ya mahabusu ya Tokyo baada ya kukaa ndani kwa zaidi ya siku 100.
Anakabiliwa na mashtaka matatu ya ufisadi kuhusu madai kuwa aliripoti kiwango cha chini cha fidia aliyolipwa na alikuwa akitaka kuhamishia hasara yake binafsi kwenye vitabu vya kampuni ya Nissan.
Hironaka alisema atakutana na mteja wake kesho kujadili kama Ghosn anatakiwa aitishe mkutano na waandishi wa habari unaosubiriwa kwa hamu.