In Summary
  • Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani wakati akizindua mradi huo na kusema utachukua miezi mitatu kukamilika.

 

Mtwara. Kaya 125 zitanufaika na mradi wa awali wa usambazaji gesi majumbani utakaogharimu Sh1.3 bilioni ambao umezinduliwa leo Ijumaa Agosti 10, 2018 mkoani Mtwara.

Hayo yameelezwa leo Agosti 10 na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani wakati akizindua mradi huo na kusema utachukua miezi mitatu kukamilika.

“Ujenzi wa mitambo hii ya awali utagharimu Sh1.3 bilioni kuwapelekea Watanzania wa awali gesi lakini litakuwa zoezi endelevu, mafundi wako eneo la mradi na shughuli za ujenzi zinaendelea. Ndani ya miezi mitatu kutoka sasa wana Mtwara mtaanza kutumia gesi majumbani,” amesema.

Dk Kalemani amesema Serikali imetenga takribani futi za ujazo za gesi 1.2 trilioni ili itumike kusambazwa majumbani kwenye kazi za kawaida, pia kuunganisha katika magari na kwamba kwa sasa tayari vituo viwili jijini Dar es Salaam na kingine shule ya Ufundi Mtwara, vimeandaliwa.

“Hivi sasa kuna magari zaidi ya 100 yanatumia gesi asilia badala ya mafuta, yote yako Dar es Salaam lakini ninataka mpango huu hadi kufikia Machi 2019 uanze na Mtwara ili na wao waachane na mafuta watumie gesi asilia,”amesema.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), mhandishi Kamulya Musomba amesema mradi huo ni mkubwa utaanzia katika mitambo ya kuzalisha umeme mjini Mtwara na mwingine utaanzia Mnazi Bay, ambao utakuwa na matoleo makubwa mawili kwa ajili ya kuzunguka mji wa Mtwara.

“Bomba la kwanza litakwenda Magereza, vitongoji mbalimbali vya Mdenga, Majengo, Chikongola, Railway, Kiyangu, Shangani, shule ya sekondarri ufundi na Chuo cha ualimu ufundi ,”amesema mhandisi Musomba

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema kuanza kwa mradi huo kutasaidia kutunza mazingira na kuwataka wananchi kuweka mazingira yatakayowawezesha kuunganishwa na wizara hiyo.

“Wizara na TPDC wamejipanga, sasa tuanze kuboresha makazi yetu na majumba yetu ili yawe na sifa ya kupata mfumo wa gesi majumbani na kuwafikia wananchi wengi,” amesema.