In Summary

Samuel Kasori, aliyewahi kuwa Katibu Myeka wa Mwalimu Julius Nyerere ameshangazwa na tabia ya wasomi nchini kukimbilia katika siasa, akihoji kuna nini wanachokifuata


Dar es Salaam. Samuel Kasori, aliyewahi kuwa Katibu Myeka wa Mwalimu Julius Nyerere ameshangazwa na tabia ya wasomi nchini kukimbilia katika siasa, akihoji kuna nini wanachokifuata.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 12, 2018 wakati akichangia mjadala katika mdahalo wa kumbukizi ya miaka 19 ya Tanzania bila Mwalimu Nyerere.

Amesema Nyerere angekuwa hai angekuwa akiwatazama  wasomi hao na kuwahurumia kutokana na jinsi wanavyopenda kusifiwa ovyo, jambo alilodai kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa akilichukia.

Amesema baadhi ya wasomi Tanzania na Afrika wanawaangusha kwa kufurahia nafasi za kuteuliwa za kisiasa.

“Tujiulize tunaoingia kwenye vyama vya siasa kule tunakwenda kutafuta nini kwa ajili ya watu wetu. Baadhi ya wasomi mmekuwa ni watu wa kujikomba komba,” amesema Kasori.

“Angalia Serikali ina maprofesa wengi wasomi wengi kwa nini walikubali nafasi hizo za kisiasa ili iweje au kutafuta nafasi za kuabudiwa.”

Amesema kwa muda aliokaa na mwalimu Nyerere alijifunza kuwa ili uwe kiongozi unahitaji msaada.

Amebainisha kuwa wasomi nchini wamekaa kimya kwa mambo mengi ikiwamo viwanda vilivyokuwepo wakati wa mwalimu Nyerere kufa.

“Mkienda huko kwenye nafasi mnazopewa mnakwenda kunyamazishwa, kuna wasomi wanatoka vyuoni haraka na kuingia kwenye siasa “amesema.

“Mwalimu hakuwa mtu wa kupenda kusifiwa sifiwa hovyo kama tunavyofanya siku hizi.”