In Summary

Kanuni hizo zilizoweka viwango vya malipo kwa wasanii kutumiwa katika maonyesho na matangazo ya kibiashara zinatakiwa zianze Julai mosi, lakini wasanii wameeleza kuwa zitaua sanaa.

 


Dar es Salaam. Wasanii na wadau wa muziki wamepinga kanuni mpya zinazotaka waandaaji wa maonyesho na wanamuziki kulipa kuanzia Sh50,000 hadi Sh5 milioni, wakisema zitaua sanaa hiyo.

Malalamiko hayo yameibuka baada ya Baraza la Sanaa la taifa (Basata) kutuma kanuni hizo katika ukurasa wake wa Twiteer la Baraza hilo, zinaonyesha mabadiliko ya viwango hivyo vya malipo vilivyotoka mwezi Februari, yataanza kutekelezwa Julai mosi.

Kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Kanuni za Basata za mwaka 2018, gharama za usajili wa wasanii na shughuli nyingine zinaanzia Sh15,000 hadi Sh50,000.

Jedwali la viwango hivyo linaonyesha kuwa gharama zimeanzia Sh20,000 hadi Sh5 milioni, ikiwa ni pamoja na kampuni au taasisi zitakazotaka kuandaa matukio ya kibiashara kutakiwa kuilipa Basata Sh2 milioni kupata kibali wakati matukio yasiyo ya kibiashara yenye kiingilio yatalipiwa Sh1.5 milioni.

Pia kutumia wasanii (branding) kwa kila tukio ni Sh5 milioni.

Nikki wa Pili, mwanamuziki wa miondoko ya rap kutoka kundi la Weusi, alisema kanuni hizo si rafiki na mamlaka haikushirikisha wadau wa sanaa kabla ya kuzitangaza.

Nick, ambaye jina lake halisi ni Nickson Simon, alisema kanuni hizo mpya haziwezi kumsaidia msanii kwa kuwa hivi sasa hawana vyanzo vingi vya mapato kama ilivyokuwa awali walipokuwa wakiuza kazi zao katika mfumo wa albamu na ziara zilizokuwa zikiandaliwa na kampuni.

“Sasa kuna biashara mbili, sisi wenyewe kuanda shows (maonyesho) zetu na pia biashara ya matangazo," alisema nyota huyo wa wimbo uliotamba wa "Hesabu" alioshirikiana na Joh Makini.

"Hivi sasa kuandaa event (onyesho) kibali (ni) milioni mbili, kibali cha ukumbi milioni moja, na bado tiketi kukatwa kodi, hapa hatutawezi.

“Katika biashara ya matangazo, kampuni ikitaka kufanya kazi na mimi itoe milioni tano kwa Basata na mimi inilipe, huoni kwamba hiyo kampuni itamchukua mtu mwingine wa kawaida, maana yake hapa chanzo kingine cha mapato kimefungwa.”

Suala hilo pia limemgusa mtayarishaji mkongwe wa muziki nchini, P Funk Majani, ambaye ameibua wanamuziki kadhaa nyota wa miondoko ya muziki wa kizazi cha kisasa.

"Zipo baadhi ya kanuni ambazo ni rafiki kwa msanii, lakini zipo nyingine si rafiki, hivyo Basata wanatakiwa kurudi kwa wadau ili kujadili upya," alisema mtayarishaji muziki huyo wa kampuni ya Bongo Records.

P Funk amesema kanuni ya kumsajili msanii, ni rafiki kwa maana inampa nguvu ya kufanya biashara, lakini ndani ya kanuni hizo kipengele cha msanii kulipiwa Sh5 milioni kila anapotumika kwenye tangazo, haiwezi kukuza sanaa.

Maoni kama hayo yalitawala mijadala katika mitandao ya kijamii ambako Basata ilitumia kutaarifu kuhusu kanuni hizo.

“Hivi Basata inatoa huduma gani kwa wasanii zaidi ya kufungia nyimbo wasizozipenda wao?” amehoji mwandishi maarufu wa vitabu nchini, Richard Mabala katika akaunti yake ya Twitter.

Mchangiaji mwingine aliyejiita Salim ameandika: “kampuni inayomkodi Diamond au Kiba kufanya tangazo, haitetereki kwa tozo ya 5M (Sh5 milioni). Wasanii wanaochipukia ambao hata kampeni hawakuwepo ndio wanaenda kufa kabisa. Hawatapata show wala tangazo.”

Mtaalamu wa mawasiliano na mwanaharakati, Maria Sarungi naye amechangia katika mjadala huo.

“Kiukweli promota au agency (wakala) gani itakuwa tayari kumlipia kiasi hicho msanii chipukizi? Msanii atapewa shilingi ngapi maana vyuma vimekaza na viingilio kukusanya si rahisi. Tutafakari #ChangeTanzania," ameandika mkurugenzi huyo wa kampuni ya Compass Communications.

Lakini katibu mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa, Godfrey Mngereza alitetea kanuni hizo kuwa zinalenga kusaidia wasanii, akisema walishirikisha wadau kabla ya kuzichapisha katika Gazeti la Serikali.

Baadhi ya vipengele vilivyoibua utata kwa wasanii na kusababisha mijadala ni malipo ya Sh5 milioni kwa ajili ya kumtumia msanii katika tangazo, gharama ambazo katibu huyo amesema zinatakiwa kulipwa na promota, au kampuni inayomtumia msanii na si msanii mwenyewe.

“Inalenga makampuni, taasisi, zinazowatumia wasanii kibiashara," alisema.

"Tunalenga sana sana namna gani wasanii waingie mkataba, kwa hiyo mkataba ndio utaonyesha kuwa kampuni hiyo inatakiwa ilipe milioni tano. Ni fedha ambazo kimsingi zinaingia kwenye mfumo wa kisheria na kikanuni kwa masuala ya fedha. Kwa hiyo haina maana kwamba itamlipa msanii, ni shughuli kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya sanaa kwa manufaa ya wasanii na wadau wa Sanaa."