In Summary

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam


Dar es Salaam. Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwapo hapo awali.

Taarifa iliyotolewa leo Mei 16, 2018  na Naibu Mkurugenzi Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu inasema makubaliano  hayo yametiwa saini jijini Dar es Salaam na mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na Rais John Magufuli, Profesa Paramagamba Kabudi na Mkurugenzi wa Tanzanite One, Faisal Juma.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Profesa Kabudi ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria amesema Tanzania One imekubali kulipa fidia Serikali kutokana na mambo iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu ulioleta hasara kwa Serikali.

Amesema fidia hiyo inatakiwa kulipwa kwa awamu; ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili kuanzia leo na haitahusisha kodi. Pia, kampuni hiyo italazimika kulioa kodi kama kawaida inazodaiwa na Serikali na tozo nyingine zote zinazodaiwa na Serikali.

Pia, Serikali imekubaliana na kampuni hiyo kuwa itafuata masharti yote ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa ni Watanzania tu ndiyo wanaoruhusiwa kuchimba madini ya vito na pale ambapo Watanzania hawana uwezo huo ndipo wanapoweza kuingia ubia na wageni.