In Summary
  • Akizungumza na wafanyakazi wa TPA leo Ijumaa Agosti 10, 2018 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema amechukua uamuzi huo kutokana na utendaji kazi wake.

Dar es Salaam. Aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko amethibitishwa  kuwa mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo.

Akizungumza na wafanyakazi wa TPA leo Ijumaa Agosti 10, 2018 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema amechukua uamuzi huo kutokana na utendaji kazi wake.

Amesema ni kawaida watumishi wa Serikali wanapoteuliwa kwenye nafasi kama hizo kukaimu ili kuangalia utendaji wao wa kazi na kama akiiridhisha mamlaka anathibitishwa.

“Kipindi  alichokaimu ameangaliwa na Serikali na bodi ya TPA kwa bahati nzuri bodi imenipa taarifa yake ya utendaji leo na nimemthibitisha,” amesema.

"Tafadhali tembo usilitie maji, nimekupandisha kwa sababu nimeona utendaji wako nina imani na wewe, usiniangushe.”

Kamwelwe amesema kuwa kuna wakati huwa anamuhurumia kutokana n kutumia muda mwingi kazini.

"Huwa nampigia simu hata saa nne  usiku na bado anakuwa yupo ofisini hadi namuuliza huwa unalala kweli. Watu kama hawa ndio tunawataka na wengine igeni mfano wake, kazi zinafanyika saa 24 ziendelee vivyo hivyo,” amesema.

Kwa upande wake, Kakoko amesema hatamuangusha waziri huyo.

“nashukuru na nitafanya kazi kadri ya uwezo wangu na kutimiza malengo ya uwepo wangu hapa,” amesema Kakoko.