In Summary

Kaimu Rais wa klabu ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again' akiwa Cape Verde amezungumzia tukio la kutekwa kwa mwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ akiwataka Wana-Simba kuwa watulivu.


Cape Verde: Kaimu Rais wa Klabu ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again' amewaambia mashabiki wa klabu hiyo kutulia baada ya tukio la mwanachama mwenzao, Mohammed Dewji 'Mo' kutekwa na ameweka wazi kuwa alimpigia simu kabla ya tukio hilo.

Try Again ni miongoni mwa wadau waliokwenda nchini Cape Verde kwa ajili ya kuiunga mkono Taifa Stars.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 11, 2018 Try Again amesema, tukio hilo ni la kusikitisha na amewaomba Watanzania hususani wanachama wa Simba watulie.

"Jambo linalotakiwa kufanywa sasa ni kumwombea dua, ili mwenzetu awe salama huko alipo na jeshi la polisi linafuatilia kwa ukaribu suala hilo," amesema Try Again.

Amefafanua kuwa, jana Jumatano, Mo alimpigia simu kuomba mawazo kwake na wakaongea kwa kipindi kirefu.

"Alikuwa na kikao cha bodi na kuna mambo aliomba nimshauri, lakini ndiyo hivyo tena," alisema.