In Summary

Leo Alhamisi Novemba 8, 2018 Rais Magufuli amepokea hati za mabalozi watatu waliochukua nafasi za watangulizi wao waliomaliza muda nchini Tanzania

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amepokea hati za utambulisho za mabalozi watatu  walioteuliwa kuziwakilisha nchi za Hispania, Canada na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini Tanzania.

Waliowasilisha hati zao za utambulisho ni balozi wa Hispania, Francisco Pedros Carretero,  balozi wa Canada Pamela O’donnel na balozi wa Umoja wa Falme la Kiarabu (UAE) Khalifa Abdulrahaman Mohamed Al-Marzooqi.

Akizungumza baada ya kupokea hati hizo leo Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amewahakikishia mabalozi hao kuwa Tanzania inathamini uhusiano na ushirikiano mzuri kati yake na nchi hizo huku akiahidi Serikali  itaendeleza na kukuza uhusiano huo kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote.

Amewaeleza Serikali inatarajia kuona shughuli mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo iliyokuwa ikisimamiwa na mabalozi waliotangulia inaendelezwa na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo uwekezaji katika viwanda, ujenzi wa miundombinu, ufadhili katika miradi ya huduma za kijamii kama vile maji, afya na nishati zikipata msukumo mkubwa zaidi.

Kwa upande wao, mabalozi hao wameahidi kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi wanazoziwakilisha na wamempongeza Rais kwa juhudi zake za kukuza uchumi, kupiga vita rushwa na kuimarisha ustawi wa jamii.