In Summary
  • Akiwa katika hafla ya kupokea ndege ya pili aina ya Airbus 220-300, Rais Magufuli amesema yuko tayari kukutana na wapinzani lakini amekuwa akisita kufanya hivyo kwa kuwa  baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakimtukana na kutishia kumchinja na kumtupa baharini.


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema yuko tayari kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ombi ambalo limekuwa likitolewa na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo viongozi wa dini.

Hata hivyo, amesema amekuwa akisita kufanya hivyo kwa sababu mara nyingi baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakimtukana na kutishia kumchinja na kumtupa baharini.

Alitoa kauli hiyo jana katika hafla ya kupokea ndege ya pili aina ya Airbus 220-300 iliyonunuliwa na Serikali na kufanya jumla ya ndege ambazo imenunua na kisha kuzikodisha kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kufikia sita.

Rais Magufuli alisema wanasiasa wamepata kitu cha kujifunza kutoka kwa viongozi wa dini hasa baada ya kuonyesha mshikamano wao katika sherehe iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda mwishoni mwa mwaka jana. Rais Magufuli alikuwa akijibu ombi lililotolewa na Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe alipopewa nafasi ya kuzungumza uwanjani hapo.

“Nimeusikia wito wa mzee Kakobe kuwa walipokutana wao kule na sisi wanasiasa tuwe tunakutana, mimi nakubali sana lakini tatizo ni kuwa huwezi kukutana na mtu anayetukana na kukuambia siku uchinjwe utupwe baharini je, siku ukikutana naye iwe ndiyo siku ya kuchinjwa,” alisema.

“Hivyo unamuacha akae peke yake, kwa hiyo mmeanza kule watu wa dini ni mwelekeo mpya wa kutengeneza Tanzania bora, uvumilivu wenu na sisi wanasiasa tukawe nao huo,” alisema.

Awali, Askofu Kakobe akitoa neno kwa Rais Magufuli alisema licha ya mambo mazuri anayoyafanya nchini lakini sio wote wanaomkubali kwa sababu hata ukifanya jambo gani zuri wapo watakaokashifu huku wakisubiri siku ya mazishi kupaza sauti zao na kusema, “Alikuwa mtu mzuri na pengo lake halizibiki.”

“Hata ikitokea umepeleka gunia 100 za mchele katika kila kaya wapo watu watakaosema huenda umewapelekea sumu. Mimi huwa ni mbishi na mpaka umeniona nimesimama mahali hapa ujue umenikosha,” alisema Kakobe.

Alisema kuna baadhi ya watu wanasema Rais anasifiwa mno na kupewa heshima zote wakati ni kodi zao walizozichangia ndizo zinazotumika katika kuleta maendeleo, “Tumelipa kodi zetu kweli lakini tunaye rubani Rais Magufuli. Japo sio wote wanakusifu ila tambua kuwa wapo watu wanaoshangilia kazi zako.”

Atoa ndege za Serikali

Katika hafla hiyo pia aliagiza ndege mbili za Serikali zipakwe rangi ya ATCL ili ziwe zinabeba abiria siku ambayo hazibebi viongozi.

Alisema badala ya ndege hizo kukaa bila kutumika, ni bora zitumiwe katika kusafirisha abiria kwenda sehemu mbalimbali ili kuhakikisha wigo wa kukuza utalii unchini naongezeka.

“Rais mwenyewe kwanza hatembei tembei kwa nini zikae zimepakiwa, hivyo ndege hizo ambazo zinabeba watu karibu 50 zibebe Watanzania kama zinaenda Musoma, Mara, Mtwara sawa. Hii itafanya ATCL kuwa na ndege za kutosha zinazofanya kazi,” alisema.

Walipa fidia

Kutokana na kuchelewa kuja kwa ndege hiyo kama ilivyokuwa katika mkataba, Rais alisema kampuni ya Bombadier imelipa Dola milioni 1.3 za Marekani.

Alisema ndege ya Airbus220-300 ya awali iliyowasili nchini na kupewa jina la Dodoma ilipochelewa ilikuwa ikilipiwa kila siku Dola 5,000.

“Ingekuwa miaka ya nyuma hizo pesa angeenda mtu mmoja akazichapa hukohuko, si ndege mmepata tusingeona kitu lakini katika utawala huu tumesema ni lazima zirudi zifanye kazi,” alisema.

Alisisitiza kuwa ndege sita zilizonunuliwa na Serikali zinamilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania na hakuna hata senti tano iliyotoka kwa mfadhili, “Hakuna kitu kizuri kama kitu kumilikiwa na wananchi na hii ni kutokana na kodi zenu mnazozitoa ndizo zinaleta maendeleo ya Taifa letu na ATCL tumewakodishia tu wakishindwa tunaweza kuwanyang’anya tukawapatia Precision Air.”