In Summary

Wakati Watanzania, Afrika Mashariki na sehemu mbalimbali duniani wakiendelea kufuatilia taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ fuatilia ili kujua mambo mbalimbali kuhusu yeye hususani maisha yake ikiwemo utajiri wake, siasa, michezo na jinsi anavyochanganyika na jamii inayomzunguuka.

Mohammed Dewji (43) alizaliwa Mei 8, 1975 mkoani Singida akiwa ni mtoto wa pili wa familia ya Gulam Dewji Hussein na Zubeda Dewji.

Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Arusha na kisha akajiunga na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya elimu ya sekondari. Mwaka 1992 alijiunga na shule ya Arnold Palmer Golf Academy iliyopo Florida nchini Marekani.

Huko aliandaliwa kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu ambayo aliyasoma katika Shule ya Saddle Brooke aliyohamia baadaye.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alijiunga na Chuo Kikuu cha Georgetown cha Washington  D.C alikohitimu Shahada ya Kwanza ya Biashara ya Kimataifa, Fedha na Theolojia.

Alirejea nchini 1998 na kuanza jukumu la kuziongoza Kampuni Tanzu za Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL) na 2000 alichukua nafasi ya Ofisa Mkuu wa Fedha na katika kipindi cha miaka 20 ya uongozi na usimamizi wake, amefanikiwa kupandisha faida na mapato ya kampuni hizo kutoka Dola 30 milioni (zaidi ya Shilingi 68 bilioni) hadi kufikia Dola 1.5 bilioni (zaidi ya Sh 3.4 trilioni).

Kampuni hizo zinazoongozwa na Dewji ambazo kwa hapa Tanzania zinachangia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa, zimetoa ajira 28,000 katika nchi 11 na zinakadiriwa ifikapo 2021, zitatoa ajira 100,000 zikijihusisha na masuala ya kilimo, masoko na simu za mkononi. Nyingine ni bima, udalali, usafirishaji, ugavi na uzalishaji wa vyakula na vinywaji.

Dewji aliwahi kuwa mbunge wa Singida Mjini 2005 hadi 2015 alipostaafu rasmi shughuli za kisiasa.

Anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola Dola 1.54 bilioni (zaidi ya Sh 3.5 trilioni) ambao unamfanya ashike nafasi ya 17 katika orodha ya watu Matajiri Barani Afrika kwa mujibu wa Jarida la Forbes.