In Summary

Mke wa Mbunda, anayeitwa Bahati anasema alijikuta tu akikubali na baadaye kumpenda mwanaume huyo

Mwanamuziki Fresh Jumbe hakukosea aliposema katika moja ya nyimbo zake, “Penzi ni kikohozi kulificha huliwezi.” Ukweli huo umejidhihirisha kwa msichana, Bahati Ramadhan (23) mkazi wa Newala mkoani Mtwara aliyefunga pingu za maisha na Jivunie Mbunda (35) ambaye ni mlemavu mwenye kimo kidogo, mkazi wa Liwale mkoani Lindi. Ndoa hiyo iliyofungwa katika Msikiti wa Mangindi uliopo mjini humo, Mei 12 mwaka huu na kuzua gumzo mjini humo na kwenye mitandao ya kijamii baada ya Mwananchi kuchapisha habari za ndoa hiyo imetoa taswira kuwa; mapenzi ni sawa na jani juu ya mti, likidondoka hutua popote.

Mwandishi wetu alipata nafasi ya kuzungumza kwa kina na wanandoa hawa, ili kujua nini kiliwasukuma husasani Bahati ambaye baadhi ya watu wanasema kitendo cha kumkubali mlemavu huyo kuwa mumewe kitampa thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mke anena

Mke wa Mbunda, anayeitwa Bahati anasema alijikuta tu akikubali na baadaye kumpenda mwanaume huyo hata kabla ya kuonana naye baada ya kupewa taarifa na jirani yake Aziza Rashid (35) kuwa kuna mwanaume mlemavu anatafuta mke wa kuoa.

“Aliniuliza uko tayari ? Nikamwambia niko tayari. Ulemavu si sababu kwangu, ilimradi ana tabia njema mimi nitaolewa naye ila kabla ya yote naomba nimuone,” anasimulia Bahati.

Bahati anasema jirani yake huyo alimpatia namba za simu za mwanaume huyo (Mbunda) na kuanza kuwasiliana naye, mwanaume alimuomba aende kwake ili waonane kuliko kuwasiliana tu kwenye simu wakati hawajaonana.

“Basi alinitumia nauli nikaenda Liwale, nikamuona kweli alikuwa ni mlemavu, sikustushwa na hali yake badala yake nilijikuta ninampenda na kwa kweli sikutaka tena kurudi nyumbani, nilikaa hapo hapo mpaka hivi leo tulipofunga ndoa,” anasema.

Jivunie anasema Aziza (mwanamke aliyewaunganisha) alikuwa jirani yake na rafiki wa karibu, aliondoka kijijini kwao mwaka 2015 na kuolewa Mtwara, hivyo Oktoba 2017 alirejea nyumbani kuwasalimia na Jivunie alimwambia kuwa anatafuta mke wa kuoa hivyo atakaporejea Mtwara akamtafutie.

“Ni kweli alikubali kunitafutia, kama utani tu siku moja akanipigia na kuniambia mwanamke amepatikana, akanipa nikazungumza naye kwenye simu. Basi tukakubaliana aje nyumbani kwangu ili niweze kumuona. Nilituma nauli akaja nikampokea,” anasema Jivunie.

“Nilipomuona siku ya kwanza, sikuamini kutokana na mwanamke mwenyewe alivyokuwa. Kwanza niseme ni mzuri. Nilipatwa na mashaka na kujiuliza kweli huyu atanikubali? Lakini kilichonishangaza tofauti na wanawake wengine, aliponiona tu akanionyesha ushirikiano mzuri.”

Jivunie anasema amewahi kuwachumbia wasichana wengi lakini kila walipoonana walionyesha uso wa dharau na wengine kumsonya na hata kumtukana wakidai hana hadhi ya kuwa nao, kitu ambacho anadai Bahati hakuwahi kumuonyesha hata siku ya kwanza walipoonana.

“Nampenda sana, ninamuona ni mwanamke wa tofauti sana, na sina shaka na upendo wake, ule ujasiri tu aliouonyesha hata baada ya kuniona na bado akasema ananipenda, kwangu hiyo ni imani tosha juu ya upendo wake kwangu,” anasema.

Hata hivyo Bahati anasema hajalazimishwa wala kushurutishwa na mtu bali amempenda mwanaume huyo kwa moyo wote kwani hata yeye ni binadamu kama walivyo wengine, anahitaji kupendwa na kuthaminiwa kama mume wa mtu.

“Nampenda mume wangu, sijalazimishwa na mtu nimeamua mwenyewe. Na ujio wangu kwake naamini niliongozwa na malaika,’’ anasema.

Bahati katalikiwa mara mbili

Katika mazungumzo yake, Bahati anadai kuwa amewahi kuolewa na wanaume wawili kwa ndoa ya Kiislamu na kubahatika kuzaa nao watoto wawili, lakini ndoa hizo hazikudumu na badala yake aliachwa kwa kila mume kumpa talaka tatu.

“Niliolewa mara ya kwanza mwaka 2011, baada ya kupata mimba mwanaume akaanza kunichukia tu bila sababu na mwisho akaniacha kwa kunipa talaka tatu mwaka 2013,” anasema.

“Mwaka 2015 nikapata mwanaume mwingine, na nikabahatika pia kuzaa naye mtoto mmoja, shida ikawa ni kipigo, alikuwa ananipiga na mwisho nikamuomba tuachane, akaniacha kwa kunipa talaka tatu,” anasema.

Anasema baada ya kuona kila mwanaume anayeolewa naye kwake ni matatizo akaamua bora amkubali Jivunie Mbunda huenda atapata upendo wa dhati kutoka kwake tofauti na wengine ambao aliwaona kuwa hawakuwa na upendo.

Suala la Bahati kuwa na historia ya kuachwa tena kwa talaka tatu kwa wanaume wawili, talaka ambayo kwa mujibu wa imani ya dini ya Kiislamu ni talaka ya kiwango cha juu yaani iliyopitiliza na inaweza kumshangaza mtu mwingine lakini kwa Jivunie hakuona ajabu.

Jivunie anadai kwake hilo halina shida kwani kwa kipindi cha uchumba wao uliodumu kwa muda wa miezi minne hajaona kasoro zozote kwa mwanamke huyo.

“Kwanza ananihudumia vizuri. Ulemavu nilionao mimi siwezi kufanya chochote bila kusaidiwa lakini yeye ananifanyia hata kuzidi ndugu zangu,’’ anasema.

Jivunie, ambaye pia ni baba wa mtoto mmoja wa kike anadai katika maisha yake amekuwa akitamani sana kumpata mke ambaye atamsaidia kumpa huduma muhimu ambazo mama ama ndugu zake hawawezi kumpa.

“Nilikuwa ninaumia sana na utu uzima wangu mama yangu kuniogesha, kunivalisha, kunipeleka msalani, ama hata ndugu yangu tu, nilitamani nipate mke na ninashukuru Mungu nimempata,” anasema. Alipoulizwa kuhusu tendo la ndoa na ulemavu wa mume wake, Bahati hakuona tabu kusema kwamba hakuna tatizo lolote na wote wanafurahia jambo hilo.

Aliyewaunganisha Bahati na Jivunie

Mwananchi ilimtafuta Aziza rafiki wa karibu na Jivunie ambaye amemtafutia mke ili kujua njia alizotumia kuwaunganisha wanandoa hawa, lakini cha kushangaza alidai kuwa ndoa yake imevunjika baada ya mume wake kuchukizwa na kitendo cha kumtafutia mtoto wa jirani yake mwanaume mlemavu.

“Ni kweli mimi niliwaunganisha, baada ya Jivunie kuniambia anataka mke wa kuoa. Cha kushangaza mimi ndoa yangu imevunjika maana baadhi ya ndugu wa upande wa mwanamke hawakupendezwa na kitendo nilichokifanya hivyo ikazua mzozo jambo ambalo lilimkwaza mume wangu akanipa talaka akidai kwa nini sikumshirikisha suala hilo,” anasema.

Aziza pia anaeleza namna alivyofanya kazi kubwa ya kumtafutia rafiki yake mke akidai kuwa alimpata msichana wa kwanza akamweleza kuwa kuna mwanaume lakini ni mlemavu akakataa ndipo alipoamua kumfuata Bahati na kumweleza.

“Nilimwambia lakini siku ya kwanza hakuweza kunijibu kitu, nikakaa baada ya siku mbili nikamfuata tena akanikubali huku akitaka nimpe namba ya Jivunie ili aweze kuzungumza naye. Nilimpatia hiyo namba wakaanza kuwasiliana,” anasema.

“Baada ya siku chache Jivunie akatuma nauli, msichana akaenda lakini nikamsisitiza nenda ukamuone kama usiporidhika naye useme mimi sikulazimishi na wala usimkubalie kwa shingo upande,”anasema.

Anasema Bahati alipofika kwa Jivunie akampokea na kukaa huko mwezi mmoja bila kurudi, hapo ndipo mzozo baina ya familia ya msichana na mume wangu ulipoanza huku kila mmoja akinituhumu kuwa kwa nini nimemtafutia mtoto wao mwanaume mlemavu.

Wazazi wa mwanamke

Shabani Mbaallu ni baba mzazi wa Bahati (bibi harusi) alipozungumza na Mwananchi anasema ameridhia kwa mikono miwili binti yake kuolewa na Jivunie baada ya binti yake kumweleza kuwa amempenda mwanaume huyo.

“Mimi binti yangu alikuja akaniambia amepata mume lakini ni mlemavu, nikasema kama umempenda mwanangu sina shida yoyote nakuruhusu ila tu ukamheshimu mumeo na kumtunza japo mwanzo niliona ugumu lakini nikakumbuka mapenzi hayachagui,”anasema.

Zainabu Ismail ni mama mzazi wa Bahati, anasema ameridhia mtoto wake kuolewa na Jivunie. “Mwanzoni nilipopata hizi taarifa kwa kweli zilinichanganya, nikaonekana kutopendezwa na mwanangu kuolewa na mlemavu lakini mume wangu aliporidhia na mimi nikaamua kukubali mwanangu aolewe,” anasema.

Ndugu wa Jivunie wanena

Mama mzazi wa Jivunie Mbunda anayeitwa Twahiba Makingito anasema ameshukuru kwa kijana wake kupata mke, kwake hiyo ni burudani moyoni.

“Sina la kuzungumza zaidi ya kusema nashukuru sana Mungu mtoto wangu amepata mke, na mke aliyempata kiukweli ana tabia njema kwa kipindi ambacho nimekaa naye hapa sijaona kasoro labda abadilike mbeleni,” anasema.

Salama Mbunda (22) ni dada wa bwana harusi ambaye pia ni mlemavu akizungumzia ndoa ya ndugu yake anasema, “Sikuamini kama kaka yangu angepata mke kutokana na ulemavu wake maana alishapata mwanamke akazaa naye lakini akakataa kuolewa naye kwa sababu ya ulemavu wake,”anasema.