In Summary
  • Kampuni ya simu za mkononi ya Halotel leo Oktoba 8, 2018 imetangaza zawadi kwa wateja wa mtandao huo ambao itawazawadia kupitia mpango wake wa ‘Longa Tusonge.’

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha miaka mitatu ya utoaji huduma nchini, Kampuni ya simu za mkononi ya Halotel imetangaza kutoa zawadi kwa wateja wake watakaotoa mawazo yatakayosaidia uboreshaji huduma kwa wateja.

Kampuni hiyo imetangaza kuanza kutoa zawadi hizo kupitia mpango wake wa ‘Longa Tusonge.’

Akizungumza wakati wa uzinduzi leo Oktoba 8, 2018, mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa kampuni hiyo, Mhina Semwenda amesema mpango huo ni sehemu ya kuthamini mchango wa wateja wake kwa kipindi hicho.

Semwenda amesema tangu kuingia kwa huduma za Halotel nchini, wamekuwa wakipata matokeo mazuri kutoka kwa wateja wanaoendelea kutumia mtandao huo.

Ameeleza kupitia mpango huo wa mwaka mmoja, wateja watapewa nafasi ya kutoa mawazo yao na yale yatakayokidhi vigezo yatapitishwa na kuwa huduma rasmi ndani ya mtandao huo.

“Lengo letu ni kuhakikisha wateja wanaendelea kupata huduma bora za mawasiliano zinazotokana na mahitaji yao katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” amesema Semwenda.

Amesema mpango huo wa Longa Tusonge ni shirikishi na nia yake ni kupokea mawazo ya wateja ili iwe rahisi kujua kitu wanachotaka kiboreshwe.

Amesema zawadi itatolewa  kwa wateja watakaotoa mawazo bora kupitia mitandao ya kijamii ya kampuni hiyo, namba ya huduma kwa wateja, maduka ya Halotel yaliyopo nchi nzima pamoja na barua pepe.

“Tunapenda kuwaalika wateja wetu walioko nchi nzima kushiriki kikamilifu katika mpango huu na sisi kama kampuni tuko tayari kuwasikiliza, kuyapokea na kuyafanyia kazi maoni yao ambayo yatazidi kuwa chachu ya kutoa huduma bora,” amesema.

Amewaahidi wateja wake kuwa Halotel itaendelea kujikita zaidi na zaidi katika kutoa huduma bora kwa wateja wake wote ikiwa ndiyo sababu kuu ya kuanzishwa kwake hapa nchini.