In Summary

Ni mwanaharakati wa kupinga ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo Wayne Lotter.

Dar es Salaam.  Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri ametaka upelelezi wa kesi ya mauaji ya mMkurugenzi na mwanzilishi mwenza wa shirika lisilo la kiserikali la Palms Foundation, Wayne Lotter (52) kukamilika mapema.

Leo Mei 17, 2018 kesi hiyo imeahirishwa tena baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Hayo yameelezwa na wakili  wa Serikali, Sada Mohamed mbele ya Mashauri wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

“Shauri hili limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema Sada.

Baada ya maelezo hayo, Mashauri ameutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wanakamilisha upelelezi kwa wakati na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 31, 2018 itakapotajwa tena.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Meneja wa Benki, Khalid Mwinyi, Rahma Almas na Mohammed  Maganga (61) ambaye ni mchimba makaburi.

Wengine ni raia wa Burundi, Nduimana Jonas maarufu Mchungaji (40) mkazi wa Kamenge Burundi, mfanyabiashara Godfrey Salamba (42) mkazi wa Kinondoni Msisiri A, mfanyabiashara Inocent Kimaro (23) mkazi wa Temeke Mikoroshini, mfanyabiashara Chambie Ally(32) mkazi wa Kia/Boma na Ofisa wa Benki ya NBC, Robert Mwaipyana (31) mkazi wa Temeke Mikoroshini.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama ya kutenda kosa na kumuua mwanaharakati Lotter.