In Summary

Malalamiko yalizidi baada ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kushindwa kuzibua daraja la barabara ya kutoka Kange Kijijini kuelekea Mkurumuzi ambalo lilikuwa limezibwa na mchanga na hivyo kuwa kikwazo cha maji yaliyokuwa yamejaa bwawani hapo.

Mwaka jana wakati kama huu baada ya kunyesha mvua zilizosababisha maafa, maeneo mengi nchini yalikuwa katika hali mbaya, kwa wakazi wa Mtaa wa Kange, Kata ya Maweni jijini Tanga wao waliilalamikia Serikali ambayo ilionekana kutoyafanyia kazi malalamiko yao ya tishio la kuliwa na mamba waliokuwa wakionekana kwenye bwawa kubwa linalotenganisha eneo la Mkurumuzi na Kange Stendi.

Malalamiko yalizidi baada ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kushindwa kuzibua daraja la barabara ya kutoka Kange Kijijini kuelekea Mkurumuzi ambalo lilikuwa limezibwa na mchanga na hivyo kuwa kikwazo cha maji yaliyokuwa yamejaa bwawani hapo.

Pamoja na Serikali ngazi ya wilaya ikiongozwa na mkuu wa wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Tanga iliyoongozwa na Martine Shigela kutembelea bwawa hilo na kisha kumtuma mtaalamu wa masuala ya wanyamapori kuwasaka mamba hao lakini jitihada za kuwatoa mamba waliodaiwa kuonekana wakati wa asubuhi wakiota jua ziligonga mwamba.

Katika kuweka tahadhari, Halmashauri ya Jiji la Tanga kupitia mtaalamu wake ililazimika kuweka vibao vya matangazo ya kuwatahadharisha watu wasisogee karibu na bwawa hilo ili wasipate madhara ya ama kuliwa na mamba au hata kujeruhiwa.

Sakata la mambo hao lililoanza Mei 2017 lilidumu kwa miezi mitatu huku malalamiko ya wananchi yakidi kutolewa.

Kilio kikuu cha wananchi walio wengi ni halmashauri hiyo kushindwa kuondosha maji katika daraja hilo.

Hata hivyo katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi baadaye malalamiko yote yalipotea baada ya wakazi wa eneo hilo kuanza kutumia fursa ya kuwepo maji hayo kwa kulima bustani za mboga, nyanya, biringanya, pilipili, bamia na wengine kufikia hatua ya kulima mahindi, shughuli ambazo zimewasaidia kumudu gharama za maisha.

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

Wakulima wengine katika bwawa hilo wamemudu kuanza ujenzi wa nyumba kutokana na makusanyo ya fedha wanazopata baada ya kuuza mboga wanazozalisha kwenye bustani kando ya bwawa hilo.

Kuwaka kwa jua kali msimu uliopita ilikuwa ni neema kwa wakazi wa Kange kwa sababu walikuwa wakitumia bwawa hilo kwa umwagiliaji wa maji kwenye bustani zao.

Miongoni mwa wanufaika wa bwawa hilo ni Geofrey Martin ambaye anasema aliamua kuanzisha butsani kando ya bwawa hilo na kuibuka kuwa miongoni mwa wauzaji wakubwa wa mboga kwa wachuuzi wanaopeleka katika masoko mbalimbali ya jijini Tanga.

Martin, akizungumza na mwandishi wa makala hii, anasema baada ya kuona maisha kwake ni magumu aliamua kushirikiana na mkewe kutumia nguvu zao kulima bustani kando ya bwawa hilo.

“Wakati naanza kulima na kumwagilia na maji ya bwawa hilo, baadhi ya watu walinicheka kuwa napoteza muda, lakini walipoona nauza na kujipatia fedha nyingi wakaniiga na ndiyo maana unaona bwawa lote kwa sasa limezungukwa na bustani,” anasema Martin.

Mkulima huyo anasema kwamba matokeo yake hivi sasa wakazi wa jiji la Tanga wanategemea kula mboga aina zote kutoka Kange pamoja na Masiwani Shamba ambapo wamejiwekea utaratibu wa kuuza kwa zamu.

Mkulima mwingine ni Luciana Mlingwa (32) ambaye anasema bwawa hilo limemsaidia kuwahudumia kwa chakula, mavazi, masomo na matibabu watoto wake watatu alioachiwa na mumewe aliyefariki mwaka juzi tofauti na kabla ya hapo ambapo kuna wakati alikosa hata uwezo wa kuwanunulia chakula.

Anasema kwamba huwa anavuna na kuuza mboga aina ya matembele, mchicha, mnavu, spinachi, maboga na bamia kwenye soko maarufu la mboga mboga la Mlango wa Chuma.

Anafafanua kwamba kuna wakati anapata hadi Sh180,000 na kwa mwezi hujipatia mmoja hujipatia wastani wa Sh720,000 na wakati mwingine hupata zaidi ya hizo, kwamba hiyo ni mbali ya mboga anayouza baada ya wanunuzi kununulia bustanini.

Hata hivyo wanasema juhudi zao zimekuwa zikidhoofishwa na magonjwa yatokanayo na wadudu wanaoshambulia mimea hasa bamia ambazo licha ya kujaribu kuweka dawa lakini hakuna mafanikio na kuomba maofisa ugani kuwatembelea ili kuwapa mbinu za kitaalamu.

Diwani atoa baraka

Diwani wa kata ya Maweni, Joseph Corvas anasema anaunga mkono hatua zilizochukuliwa na wakulima wa mboga wa Kange katika kutumia maji ya bwawa hilo kwa sababu wamejiongeza baada ya kuona fursa imewafuata walipo.

“Kwa sasa sipigiwi tena simu na wakazi wa eneo hilo kulalamikia maji hayo, nadhani ukiwaambia tunataka kuzibua daraja ili yatoke utazua ugomvi na malalamiko ambayo si rahisi kuyatatua,’’ anasema Diwani Corvas.

Diwani huyo hata hivyo anasema mipango ya halmashauri kuzibua daraja ili maji yapite ipo pale pale na kwamba likipatikana fungu kazi hiyo itafanyika.

“Wakati ule niliwaambia wakazi wa eneo hilo kwamba kuna mwekezaji aliyeahidi kutengeneza daraja linalozuia maji kupita na kwamba mipango ya halmashauri bado ipo pale pale,’’ anasema.

Anasema kitendo cha wakazi wa Kange kuamua kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa maji ya bwawa hilo kimesababisha ajira ya vijana ambao kama lisingekuwepo wangejikuta wakishiriki vitendo vya kihalifu ili kujipatia fedha.

“Rais John Magufuli amesema wenye juhudi wataishi maisha mazuri lakiniwavivu wataiona Serikali yake mbaya, hili limedhihirishwa na wapiga kura wangu wa Kange walioamua kujiongeza kwa kutumia fursa ya maji,” anasema Corvas.

Wauzaji wa mboga sokoni

Wauzaji mboga wa soko la Mlango wa Chuma wamesema mboga kutoka Kange ndiyo iliyowalisha wakazi wa Tanga katika kipindi kilichopita cha jua kali lililosababisha kuadimika kwa mboga.

“Kama si mboga za Kange kipindi kile cha jua biashara ya kutembeza majumbani ingekuwa ngumu kwa sababu ukame ulisababisha washindwe kulima kabisa,” anasema Hadija Dafa anayetembeza mboga mitaa ya Chumbageni, Chuda na Kisosora.

Wakazi jirani na bwawa waonya

Wakizungumzia kuhusu hatari ya mamba, wakazi wa eneo la jirani na bwawa hilo wanasema bado wapo kwa sababu kuna wakati huibuka na kuonekana wakiota jua.

“Hatari ya mamba hapa bado ipo ni vyema hata kama maji hayataondolewa lakini wataalamu wafanye kazi ya kuwaua badala ya kusubiri watu hasa watoto wauawe au hata kupata madhara mengine,’’ anasema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.