Ukizungumzia Fastjet hapa nchini ni dhahiri watumiaji wengi wa usafiri wa anga watakuwa wanalitambua shirika hilo.

Kabla ya shirika hilo kusitisha shughuli zake, lilikuwa limetawala soko la ndani katika usafiri wa ndege kwa asilimia 45.

Awali, Fastjet Tanzania ilikuwa ikiitwa Fastjet PLC ambayo ni kampuni ya ndege ya Uingereza na Afrika Kusini inayofanya kazi ya usafirishaji ndani ya Afrika.

Uendeshaji wa kampuni hiyo ulianza kwa kutumia jina la Fly540 na nchini ilianza safari zake Novemba 2012.

Fastjet PLC, ilijiondoa mapema mwaka jana na shirika hilo hivi sasa linamilikiwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha ambaye ana hisa asilimia 68 huku mmiliki mwenza akiwa ni Hein Kaiser wa Afrika Kusini.

Tangu kuanza kwake, kampuni ilibainisha lengo lake la kutoa huduma kwa gharama ndogo zaidi Afrika na hilo lilitekelezwa kwa vitendo hapa nchini.

Watanzania wengi hususan wanaosafiri kwa ndege katika safari zao za ndani watakubaliana nami kuwa Fastjet ndilo shirika nafuu zaidi na huenda wengi waliopanda ndege kwa mara ya kwanza walisafiri kwa ndege zake aina ya Embraer 190.

Hivi sasa shirika hilo limezuiliwa kufanya shughuli zake kwa kuwa halijatimiza baadhi ya matakwa ya kisheria.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Desemba 17 ilitoa notisi ya siku 28 ya kusudio la kufuta leseni ya shirika hilo endapo halitatimiza matakwa ya kisheria.

Notisi hiyo ilieleza kuwa mwenendo wa shirika hilo hauridhishi kwa kuwa halina ndege baada ya ndege yake aina ya Boeing 737-500 kuzuiliwa kufanya safari kutokana na hitilafu za mara kwa mara jambo ambalo linasababisha usumbufu kwa abiria.

Kadhalika, TCAA ilibainisha kuwa shirika hilo halina meneja wa operesheni ambaye ni mtaalamu wa operesheni na matengenezo ya ndege.

Pia, lilielemewa na madeni lakini pia lilikuwa halijawasilisha mpango wake wa kibiashara na kifedha tangu kujiondoa kwa Fastjet PLC.

Hivi karibuni, Fastjet Tanzania walitaka kuingiza ndege mbili aina ya Boeing 737-500 lakini hawakuruhusiwa kwa sababu ambazo TCAA ilieleza kuwa ni kuchelewa kuwasilisha maombi ya kuingiza ndege hizo.

Hata hivyo, TCAA imeeleza kuwa tayari shirika hilo limewasilisha maelezo ya baadhi ya matakwa ya notisi na inayafanyia kazi ili kutoa majibu lakini endapo hawataridhika, kulingana na matakwa leseni ya shirika hilo itafutwa.

Natambua kuwa usafiri wa anga ni jambo nyeti na usipodhibitiwa unaweza kuhatarisha usalama na kugharimu maisha ya watu lakini kwenye suala la madai sheria inaweza ikapindishwa ili kuliokoa shirika hilo ili mradi lieleze mpango wake wa ulipaji wa madeni.

Nasema hivyo kwa sababu, Fastjet inahitaji kushikwa mkono kwanza.

Shirika hilo limeomba msaada wa Serikali likitaka liruhusiwe kuendelea na usafirishaji ili liweze kulipa madeni yanayolikabili ambayo kwa mujibu wa TCAA, yanakadiriwa kufikia takriban Sh6 bilioni.

Pili, shirika hilo lilikuwa linatumiwa na Watanzania wengi, lilipozuiliwa kufanya safari zake, abiria waliokuwa wamekata tiketi ilibidi warudishiwe nauli zao, baadhi wamerudishiwa na wengine bado.

Shirika hilo linasema fedha zimekwisha kwa kuwa nyingi zilitumika kukodi ndege ili kurejesha huduma.

Wapo abiria ambao muda wao wa safari bado haujafika, Fastjet wanasema lengo lao ni kuwasafirisha wateja wake lakini siyo kuwarudishia nauli zao, hivyo msisitizo umekuwa kuruhusiwa kuingiza ndege zao na kuendelea na biashara badala ya kukazania wawarudishie nauli abiria.

Kusitishwa kwa shughuli za Fastjet ni wazi kuwa kuna baadhi ya wasafiri wa anga sasa watarudi katika usafiri wa mabasi kwa kuwa wengi walifuata urahisi wa nauli ambao ndiyo ilikuwa nguzo ya shirika hilo.

Pia, Serikali imekuwa ikipiga debe wazawa kumiliki uchumi wa nchi kwa kushiriki katika uwekezaji kwenye sekta ambazo awali wengi walidhani ni kwa ajili ya wageni na Serikali.

Fastjet ikiwa ni kampuni ya mzawa, inapaswa kusaidiwa ili iinuke na kuendelea kutoa huduma kwa wateja wake lakini pia kuinua sekta ya usafirishaji, uchukuzi, utalii na kukuza mawasiliano kwa kuwa kutakuwa na wepesi wa kutoka eneo moja kwenda jingine.

Juhudi za kuwalinda wawekezaji na mitaji yao hazitakuwa zimeanzia kwa shirika hilo, hatua hizo zimekuwa zikichukuliwa ili kukuza uwekezaji nchini.

Ephrahim Bahemu ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi, anapatikana kwa namba; 0756-939401