In Summary

Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania,  Dk Hamisi Kigwangalla ametangaza marufuku ya kusafirisha viumbe hai nje ya nchi.

Dodoma. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema hakuna viumbe hai watakaosafirishwa nje ya Tanzania, hata iwe kunguni au chawa.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 24, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya wizara yake mwaka 2019/2020, kubainisha kuwa kitendo cha kusafirisha wanyama hakiungi mkono hivyo asingependa ifanyike akiwa katika wadhifa huo.

"Mimi huwa simung'unyi maneno,  nasema katika kipindi ambacho nitakuwa madarakani sitaruhusu hata chawa au kunguni isafirishwe nje ya nchi. Hilo nitalisimamia kwa nguvu zote," amesema Kigwangalla.

Amebainisha kuwa kinachotakiwa kufanyika kwake katika suala hilo ni kutoa vibali kwa wananchi ambao watakuwa na nia ya kuanzisha ufugaji wa wanyama (Zoo)  ili wanaotaka wakaagalie huko.

Wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti hiyo mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa aliibua hoja ya fidia kwa wafanyabiashara wanaosafirisha wanyama nje ya nchi, akisema walipata hasara kubwa wakati sheria bado ipo.

Pamoja na michango mingi ya wabunge lakini  Dk Kigwangalla alishikilia msimamo wake kuwa hana shina na fidia hivyo watalipwa wakati utakaofaa.

Hoja hiyo kuhusu wafanyabiashara ilizua mvutano lakini Dk Tulia aliifunga kwa kuwataka walioingia mkataba kama hawaridhiki na alichosema Waziri wanaweza kwenda mahakamani.