In Summary

Wakati dirisha la uombaji wa mkopo wa elimu ya juu kwa njia ya mtandao likitarajia kufunguliwa Julai mosi, 2019 waombaji wameaswa kutumia dakika 30 kukamilisha maombi katika mfumo ikiwa ana nyaraka zote muhimu zinazohitajika.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi ya Elimu ya Juu (HESLB) nchini Tanzania inatarajia kufungua dirisha la kutuma maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao Julai mosi 2019 na kufungwa Agosti 15,  2019.

Mbali na kufungua dirisha hilo pia limebainisha bodi hiyo inawasiliana na Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuweka utaratibu bora wa kuwawezesha wanafunzi wahitaji waliopo katika kambi za JKT kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandao.

Taarifa ya Bodi hiyo iliyotolewa jana Jumanne Juni 25, 2019 na Mkurugenzi Mtendaji wake, Abdul-Razaq Badru ilisema kutokana na dirisha kukaribia kufunguliwa wanafunzi wanashauriwa kuhakikisha wanakamilisha nyaraka muhimu zinazohitajika na kutumia dakika 30 kukamilisha maombi hayo.

“Mwombaji anatakiwa kuambatanisha nakala ya cheti cha kuzaliwa cha mwombaji iliyothibitishwa na Rita au wakala wa Usajili wa matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA), nakala ya cheti cha kifo cha mzazi wa mwombaji iliyothibitishwa na Rita au ZCSRA.”

“Barua ya mganga mkuu wa Mkoa, wilaya au hospitali ya manispaa, wilaya, au jiji inayothibitisha ulemavu wa mwombaji au mzazi wake na barua kutoka taasisi iliyofadhili masomo ya sekondari au stashahada ya mwombaji mkopo,” amesema Badru

Amesema, “Mfumo wa uombaji mkopo kwa njia ya mtandao utakaofunguliwa haumlazimishi mwombaji kuwa na matokeo ya kidato cha sita bali atapaswa kuwa na namba ya mtihani wake wa kidato cha nne.”