In Summary

Kocha wa Croatia, Zlatko Dalic, aliwashukuru wachezaji wake hao wazoefu 

Moscow, Russia. Ingawa wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya England na kutinga fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia, wachezaji wa Croatia, bado hawaamini katika hilo.

Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo wachezaji wa Croatia walisema hawajui waseme nini kwa sababu wamepata zaidi ya kile walichokusudia ambapo malengo yao yalikua kufika 16.

Hii inatokana na maandalizi yao pamoja na uchanga wa wachezaji wao wengi, kwani ukimuondoa nahodha Luka Modric, 32, Ivan Rakitic, 30, Ivan Perisic, 29 na mfungaji Mario Mandzukic, 32, wengine wote ni chipukizi na hawana uzoefu wowote wa mechi za kimataifa.

Kocha wa Croatia, Zlatko Dalic, aliwashukuru wachezaji wake hao wazoefu akisema wameliletea taifa lao heshima kwa kufika fainali ya Kombe la Dunia nchi hiyo iliyojitangazia Uhuru, Juni 25, 1991 baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Yugoslavia.

“Bila shaka uzoefu wa wachezaji wetu viongozi akina Modric, Rakitic, Perisic na Mandzukic umetusaidia tumefika mahali ambapo wengi hawakutarajia, tunashakuru sana na kuwapongeza tunaamini watatuongoza kutwaa ubingwa,” alisema Dalik.

Alisema hawana cha kupoteza katika mchezo wa fainali utakaiopigwa Jumapili hii dhidi ya Ufaransa, baada ya kutofanikiwa kutinga fainali hizo mwaka 1998, walipong’okewa katika hatua ya nusu fainali, hivyo wameweza kuandika historia kwa kufika fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia katika historia yake.

Wakati Croatia ikicheza fainali yake ya kwanza, Ubelgiji iliyoichapa England bao 1-0 katika mechi ya mwisho ya makundi itarudiana nayo tena Jumamosi hii katika mchezo kusaka mshindi wa tatu.