In Summary

Maalim Seif alisema hayo katika taarifa yake aliyoituma Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki, akisema ukomo wa Rais wa Zanzibar kikatiba unamalizika kesho.

Zanzibar: Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amewasilisha malalamiko yake katika jumuiya ya kimataifa kuhusu tamko la kufutwa Uchaguzi Mkuu, akidai iwapo hadi kesho hakutakuwa na suluhisho atawaachia wananchi waamue.

Maalim Seif alisema hayo katika taarifa yake aliyoituma Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki, akisema ukomo wa Rais wa Zanzibar kikatiba unamalizika kesho.

Alidai kuanzia hapo Zanzibar itakuwa haina Serikali na ikifikia hatua hiyo, maana yake kutaibuka mgogoro wa kikatiba.

Maalim Seif katika waraka huo alisema hadi leo kama kutakuwa hakuna hatua za kumalizia kutoa matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi na kuheshimu demokrasia, viongozi wa CUF akiwamo yeye (Maalim Seif) watajiondoa katika jambo hilo na kuwaachia wananchi waamue.

Alisema anaamini jumuiya ya kimataifa na Watanzania wapenda amani na wanaoheshimu haki za binadamu wataungana na Wazanzibari katika hili.

Maalim Seif alisema tangu kuibuka kwa tatizo hili Oktoba 28, baada ya Jecha kutangaza kufuta matokeo, amefanya juhudi za kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete zimeshindikana baada ya kukosa ushirikiano toka kwa wasaidizi wake, pia juhudi za kuonana na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein nazo zilishindikana.

Alidai kwenye waraka huo kwamba kuna taarifa wamezipata toka Pemba kwamba ZEC, imewaita viongozi wote wa CCM na kuwataka wapinge matokeo.

Maalim Seif katika waraka wake pia alieleza kushangazwa na kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuridhia kura za majimbo 18 ya Pemba ambayo ZEC inasema kuna kasoro nyingi ikiwamo idadi kubwa ya wapiga kura ikilinganishwa na idadi halisi.

Wakati huo huo, chama cha CUF kimeahidi kuongoza nchi katika hali ya umoja, maridhiano kwa kushirikiana na viongozi wa CCM chini ya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Makao Mkuu wa CUF, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema hakuna haja ya kuonyesha hofu kuhusu uongozi wa Maalim Seif, kwani ataiongoza nchi kwa misingi ya haki na uadilifu.

“Chama chetu kinawahakikishia Wazanzibari wote kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na Maalim Seif itakuwa ni Serikali ya wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, dini au asili ya mtu anapotoka.

“Kinachosubiriwa kwa hamu, ni matokeo ya mwisho kutangazwa na ZEC, tukiamini kuwa Mgombea wetu ndiye mshindi,” alisema.

Alisema katika kutekeleza ahadi zake hizo, Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoshirikisha vyama vya CUF na CCM chini ya Maalim Seif itasahau yote yaliyopita na kwamba itashajiisha maridhiano na masikilizano miongoni mwa wananchi na haitofufua makaburi kwa kulipiza visasi” aliahidi Naibu Katibu Mkuu huyo.