In Summary

Mkurugenzi huyo mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku pia ametaja yanayojitokeza baada ya upigaji kura kuwa miongoni mwa mambo yanayopaswa kutatuliwa kikatiba


Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji ti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema ni vyema yakawepo mabadiliko ya Katiba kwa sababu wananchi hawaridhishwi  na mambo yanayoendelea katika chaguzi mbalimbali nchini.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 12, 2018 akichangia mjadala katika mdahalo wa kumbukizi ya miaka 19 ya Tanzania bila Mwalimu Julius Nyerere.

Mdahalo huo uliopewa jina la ‘mienendo ya chaguzi na mustakabali wa mataifa ya Afrika’, umehusisha wanasiasa, wasomi wa watu wa kada mbalimbali.

Butiku amesema kila mara baada ya wananchi kupiga kura kunakuwapo na vurugu zinazosababishwa na viongozi ambao wanajulikana, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Ipo haja ya kuitizama Katiba Mpya ili kujirekebisha kutokana na mienendo ya uongozi iliyopo,” amesema Bujiku.

Amesema binadamu wana hulka ya kujitutumua, kupenda vyeo na kwa kawaida wanapokuwa wengi kunakuwa na utaratibu wa kuwaongoza.

“Katiba iliyokubaliwa na wananchi baadaye ikapelekwa kwenye Bunge Maalumu, ndio ina majibu ya maswali yote haya, ”amesema Bujiku.