In Summary
  • Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo nchini(TIB), Charles Singili ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Taasisi za Fedha za Maendeleo za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC DFI).

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Charles Singili ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Taasisi za Fedha za Maendeleo za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC DFI).

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Januari 8, 2019 jijini Dar es salaam, Singili amesema kamati ya uongozi ya mtandao huo ilimteua kutumikia nafasi hiyo Desemba, 2018 na uteuzi wake utadumu hadi Desemba 2020.

Amesema majukumu yake katika nafasi hiyo ni pamoja na kuhamasisha ushirikiano katika miradi, utafutaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusaidia uwekezaji wa mitaji na uwekezaji wa pamoja katika miradi.

"Ziko faida nyingi za uteuzi huu, kwanza TIB itashirikiana na taasisi nyingine nchini kujenga mazingira wezeshi kwa Tanzania, kuhakikisha taasisi zinapata fedha za kutosha katika miradi yenye maslahi ya kikanda kama vile miundombinu ya usafiri, nishati, maji inapata fedha za kutosha," amesema Singili.

Mwaka 2002, mawaziri wa nchi za SADC waliunda kamati ndogo ya taasisi za fedha za maendeleo ya Jumuiya ya SADC(SADC DFI subcommittee).

Kamati hiyo inajumuisha taasisi mbili ambazo ni mtandao wa SADC DFI wenye wanachama 41 pamoja na Kituo cha Rasilimali cha Taasisi za Fedha za Maendeleo (SADC DFRC).

Kwa hapa nchini, benki mwanachama katika mtandao huo ni benki hiyo ya Maendeleo (TIB), Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).