In Summary
  • Mwanaharakati, Bob Wangwe amesema ameanza kufuatilia fedha zake zilizolipwa baada ya kuhukumiwa kwenda jela ili zirudishwe kwa sababu ameshinda rufaa dhidi ya kesi hiyo.

Dar es Salaam. Mwanaharakati wa utawala bora, Bob Wangwe amesema ameanza mchakato wa kufuatilia malipo ya Sh5 milioni alizolipa kama mbadala wa kwenda jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na miezi sita.

Wangwe alikabiliwa na kesi ya uchochezi kupitia mtandao wa kijamii baada ya kutoa maoni yake kwamba uchaguzi wa Zanzibar haukuwa huru na haki kutokana na mambo mbalimbali yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo.

Akizungumza kwenye kongamano kuhusu ushiriki wa wananchi kwenye uongozi wa nchi lililofanyika jana Juni 25, 2019, Wangwe alisema baada ya hukumu ile aliamua kulipa faini hiyo ili asiende gerezani.

Alisema baada ya kukamilisha malipo hayo, hakuridhika, akakata rufaa. Amesema Machi mwaka huu alishinda rufaa yake na kufutiwa hatia. Amesema ataendelea kufuatilia ili fedha zilizolipwa zirudishwe.

“Nimeshinda rufaa ile, sasa nimeanza kufuatilia ili fedha zile zirudishwe. Ni fedha ndogo lakini nataka zikafanye shughuli nyingine za maendeleo,” amesema Wangwe wakati akielezea uhuru wa kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii.