In Summary
  • Katika kupunguza unene, teknolojia nayo inaendelea kufanya biashara ikiwalenga wale wanaotaka kupunguza uzito. Kwa mfano, Application ya 7Minute Workout and Water Drink Reminder imepata umaarufu zaidi na inapakuliwa na mamilioni ya watu duniani kwa njia ya simu.

Dar es Salaam. Kwa kile kinachoonekana kuwa tatizo la unene kupita kiasi limekuwa kubwa nchini, kumekuwapo na ongezeko la biashara ya kupunguza unene.

Biashara hizo zinazotangazwa kwa kiasi kikubwa katika mitandao ya kijamii zikieleza namna ya kupunguza unene, zinatekelezwa kwa njia tofauti - baadhi kwa tiba, zingine kwa mazoezi na zipo pia ambazo mtu anaingizwa kwenye programu maalumu bila kuacha kula wala mazoezi.

Mtandao wa Detail.com unaeleza kuwa asilimia 45 ya Wamarekani wamejiwekea malengo ya kupunguza unene mwaka huu.

Ingawa hakuna takwimu sahihi hapa nchini, lakini utafiti uliofanywa na Mwananchi umebaini wanaofanya biashara ya dawa za kupunguza unene wanapata wateja wengi.

Kwa mfano, mtandao wa WhatsApp wa Semgogwe, dawa ya kupunguza uzito kuna wanachama 299 ambao wote wamenunua dawa hiyo ya kupunguza uzito. Wafanyabiashara pia wamefungua makundi ya WhatsApp ili kuwaweka wateja wao na kuwashawishi zaidi kununua bidhaa hizo.

Mtandao mwingine wa Instagram uitwao Weightloss Challenge unatangaza kuwa unasaidia kupunguza unene bila mhusika kujinyima kula, kumeza vidonge na hakuna mazoezi, bali wanatumia lishe salama na miongozo rahisi.

Wafanyabiashara hao wanatumia pia akaunti za watu maarufu kutangaza biashara zao. Kwa mfano, pindi tu anapotuma ‘post’ msanii maarufu nchini, basi wafanyabiashara zaidi ya wanne au watano wanatangaza biashara zao za kupunguza unene.

Dawa hizo za kupunguza unene zinauzwa kati ya Sh15000 hadi 100,000.

Lakini kwa wanaotaka kutumia lishe na ushauri ili kupunguza uzito, wapo wafanyabiashara wanaotumia mafunzo. Wao hutoza gharama za mafunzo pekee. Kwa mfano, katika mafunzo ya siku 21 mtu anaweza kupungua kilo nne hadi saba ambapo mteja analipia Sh50,000 hadi 100,000 kwa miezi sita.

Pia kuna maduka ya mitandaoni kama Health U, ambayo yanauza bidhaa za kupunguza uzito. Kwa msaada wa teknolojia, wateja wengi wananunua dawa hizo kwa njia ya mtandao na kufikishiwa mpaka nyumbani. Joram Mushi, mkazi wa Mbeya anasema ameagiza dawa ya kupunguza unene iitwayo Glucomannan kwa njia ya mtandao huo na kupelekewa hadi ofisini kwake.

Mfanyabiashara wa vipodozi eneo la Sinza Madukani, Sifa Mwambipi alisema kuna sabuni ambayo inatumika kwa kupaka kwenye tumbo ili ilete matokeo mazuri inatakiwa kuogewa mara mbili kwa siku kwa miezi mitatu ambayo pia ipo mtandaoni.

Gym na vituo vya afya

Pamoja na dawa za kupaka au kumeza, pia vituo vya kufanya mazoezi vimeendelea kufunguliwa na kutangazwa katika mitandao ya kijamii. Vituo hivyo vinatangaza kuwasaidia wale wanaohitaji kupunguza vitambi.

Mitandao hiyo inawalenga zaidi wanawake wanaotaka kupunguza tumbo na wanaotaka kuongeza makalio na ‘hips’. Mfano hii ni mtandao wa You Tube’ wa Tanzanes Gym, inayotoa mafunzo kwa njia ya mtandao na kuwahimiza watu kujiunga.

Teknolojia yazidi kupaa

Katika kupunguza unene, teknolojia nayo inaendelea kufanya biashara ikiwalenga wale wanaotaka kupunguza uzito. Kwa mfano, Application ya 7Minute Workout and Water Drink Reminder imepata umaarufu zaidi na inapakuliwa na mamilioni ya watu duniani kwa njia ya simu.

Desemba mwaka jana, kampuni ya Samsung ilitambulisha App ya Galaxy Gear S2 ambayo inarekodi mazoezi ya mwili anayofanya mtumiaji kwa kupima kiasi cha hatua za mtembea kwa miguu na kupima mapigo ya moyo.

Simon Kariithi, mkuu wa kitengo cha biashara ya mtandao wa kampuni ya Samsung kwa Afrika Mashariki anasema App hiyo inasaidia kupunguza unene na inarekodi data za kiafya kwa saa 24.