In Summary
  • Benki ya I&M imefanya droo ya tatu ambayo ni ya mwisho na kutangaza washindi watano wa poromosheni ya 'Jidabo na I&M Bank' na kufanya jumla ya washindi hao kufikia 15.

Dar es Salaam. Benki ya I&M imefanya droo ya tatu ambayo ni ya mwisho na kutangaza washindi watano wa poromosheni ya 'Jidabo na I&M Bank' na kufanya jumla ya washindi kufikia 15.

Meneja Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Emmanuel Kiondo leo Jumanne Januari 8, 2019  amesema lengo la kuendesha promosheni hiyo ni kuwazawadia wateja wao kwa kupata mara mbili ya fedha walizokuwa nazo kwenye akaunti zao.

Kiondo amesema benki hiyo ilitenga kiasi cha Sh75 milioni kwa ajili ya kuwazawadia wateja wake hao.

Amesema kila mshindi hupata mara mbili ya akiba iliyopo kwenye akaunti yake hadi kufikia kiasi cha juu cha Sh5 milioni.

"Kampeni hii ilizinduliwa mwanzoni mwa Oktoba mwaka jana hivyo imedumu kwa muda wa miezi mitatu ambapo kila mwezi tumekuwa tukipata washindi watano na kutangazwa," amesema Kiondo.

Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo, Donald Matte amewatangaza washindi hao watano waliopatikana leo kuwa ni Poulomi Hemlata, Jenipher Mtei, Thomas Malisa, Kefren Bohongo na UniSoft Technologies (T).

Baada ya Matte kuwatangaza washindi hao, Kiondo alibainisha kuwa ili kushiriki mteja alipaswa kufungua akaunti ya akiba, akaunti ya biashara, akaunti ya mshahara ama akaunti ya mtoto katika tawi lolote la benki hiyo katika kipindi cha promosheni.

Kwa mteja ambaye tayari alikuwa na akaunti alipaswa kuhakikisha ana akiba ya Sh200, 000 ikiwa anamiliki akaunti ya biashara au Sh100,000 ikiwa anamiliki akaunti nyingine zinazohusika katika promosheni hiyo.

Benki ya I&M iliingia nchini Tanzania mwaka 2010 baada ya kuinunua benki iliyokuwa ikijulikana kama CF Union ambayo ilianzishwa mwaka 2001.