In Summary

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM) Hussein Bashe  amezungumzia changamoto zinazowakabili wakulima wa mazao ya biashara na chakula akiitaka Serikali kuchukua jukumu la kuwasaidia pale wanapokumbana na hasara

Dodoma. Mbunge wa Nzega Mjini (CCM) Hussein Bashe amesema anaona kuna tatizo kubwa sana serikalini na ama mawaziri na wataalam wamekataa kufikiri ama wameamua kutegeana.

Bashe ameyasema hayo bungeni leo Alhamisi Novemba 8, 2018 wakati akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka wa fedha 2019/20  uliowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango Jumanne iliyopita.

“Mimi naona kuna tatizo kubwa sana serikalini, ni kwamba mawaziri na wataalamu labda wamekataa kufikiri, ama wameamua kutegeana,” amesema.

“Najiuliza tumbaku inaporomoka, soko kubwa sasa la tumbaku lingekuwa Mashariki ya Kati, tunaambiwa tupunguze production (uzalishaji). Leo korosho tunaenda kwenye matatizo, nataka nishauri, sisi hatuwezi ku-control soko la dunia, tuna control na volume za ndani ili tuweze lazima tuweze kutoa motisha.”

Bashe ameomba Serikali watakapokuja na mwakani waje na namna ya kuanzisha mfuko huo wa kunusuru wakulima na namna ya kurekebisha kodi.

Amesema asilimia 60 mpaka 70 ya wananchi ni wakulima na kwamba hao ndio waendeshaji na waanzisha viwanda.

“Tunajenga reli ambayo itabeba bidhaa, tunajenga barabara ambayo itabeba bidhaa na binadamu, leo mazao ya chakula na ya biashara yote yanaanguka kwa sababu za nje na kwa sababu za ndani,” amesema.

Amesema hatua ya  kwanza inayotakiwa kufanywa ili kuokoa sekta ya kilimo ni kuja na mpango wa kuanzisha mfuko wa kuwalinda wakulima na hasara za bei ambao utafidia hasara zinazowakabili wakulima.