In Summary
  • Mnada huo unafanyika baada ya Mahakama Kuu ya New York kufuta kesi aliyoifungua Madonna kwa ajili ya kumzuia rafiki yake, Darlene Lutz asiuze barua hiyo  iliyoandikwa kuhusu kuvunjika uhusiano wake na Tupac na vitu vingine.

 Mnada wa barua za kuvunjika kwa mapenzi kati ya mwanamuziki maarufu duniani, Madonna Louise na marehemu Tupac Shakur, utafanyika Julai mwaka huu.

Mnada huo unafanyika baada ya Mahakama Kuu ya New York kufuta kesi aliyoifungua Madonna kwa ajili ya kumzuia rafiki yake, Darlene Lutz asiuze barua hiyo  iliyoandikwa kuhusu kuvunjika uhusiano wake na Tupac na vitu vingine.

Jaji wa New York, Gerald Lebovits alitupilia mbali kesi ya Madonna dhidi ya Lutz akisema kuwa muda wa kuvipata vitu hivyo umekwisha

Mojawapo ya vitu hivyo ni barua ya kuvunjika kwa uhusiano kati yake na msanii Shakur aliyefariki 1996 ambaye alikuwa na uhusiano wa kisiri na Madonna.

Kwa mujibu wa mtandao wa burudani wa TMZ, mnada huo sasa utafanyika mwezi Julai.

Madonna alidai kwamba hakujua kwamba Lutz alikuwa akimiliki barua za Tupac alizoandika 1995 hadi aliposikia kuhusu mnada huo wa mtandaoni mwaka uliopita.

Katika barua hiyo iliyojaa hisia, msanii huyo wa rap alimwambia Madonna kwamba kuwa na uhusiano na mtu mweusi kutamsaidia katika kazi yake na kwamba, sura yake itaharibika iwapo ataanza uhusiano na mtu mweupe.

Wapenzi hao walikuwa katika uhusiano wa kisiri ambao ni hivi majuzi ambapo Madonna alikubali kutangaza wazi.

Jaji Gerald Lebovits alisema katika uamuzi wake siku ya Jumatatu kwamba nyota huyo wa muziki wa Pop hawezi tena kumshtaki rafiki yake huyo .

Madonna aliiambia mahakama mwaka uliopita wakati alipojaribu kuzuia mnada wa vitu hivyo kwamba, umaarufu wake haukumpatia uwezo wa kutaka kuhifadhi hati yake ya faragha ikiwemo vitu kama hivyo.