In Summary

Mwanaume huyo anadaiwa kutekeleza mauaji hayo kutokana na ugomvi wa kifamilia.

 Baba anayedaiwa kuwaua watoto wake mapacha kwa kuwakata vichwa Respicius Deogratias mkazi wa kijiji cha Butahyaibega Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera amekamatwa leo jijini Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustine Ollomi amesema baada ya msako mkali, mtuhumiwa ametiwa mbaroni leo Aprili 16 baada ya kutoroka na taratibu za kumsafirisha ili akabiliane na mashitaka zinafanyika.

Amesema kuwa usiku wa kuamkia April 15, mtuhumiwa anadaiwa kuwaua watoto wake mapacha, Nyangoma na pacha mwenzake Nyakatto ambapo baada ya mauaji hayo mtuhumiwa alitoroka.

Kamanda Ollomi amesema tukio hilo la kutisha limegubikwa na mambo mengi ya uvumi na kuwataka wananchi watulie hadi uchunguzi unaoendelea utakapokamilika.

 

"Hili si tukio la kawaida kuna mambo mengi yanavumishwa lakini wananchi watulie na Polisi tunachunguza kiini cha tukio hilo, taratibu za kumsafirisha mtuhumiwa kutoka Mwanza zinaendelea,"amesema Kamanda Ollomi

Hata hivyo hakuwa tayari kufafanua kwa undani eneo alipokamatwa mtuhumiwa na kama alikuwa mafichoni na badala yake alisema Polisi ina mtandao mrefu wa kunasa wahalifu.

Awali Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bulambizi Dickson Barongo alisema kuwa usiku wa kuamkia Jumatatu wananchi wa kijiji cha Butahyaibega waliungana na kuendesha msako dhidi ya mtuhumiwa ambapo walifunga njia zote zinazoingia na kutoka.