In Summary
  • Askari Magereza, Sajenti Yohana Tangawizi amejiua kwa kujipiga risasi mbili mdomoni na kuacha ujumbe unaodai amechukua uamuzi huo kutokana na kuugua muda mrefu.

Serengeti. Askari Magereza Yohana Tangawizi wa Gereza la Mradi Tabora B wilaya Serengeti mkoani Mara amejiua kwa risasi nyumbani kwake.

Mganga Mkuu wa hospitali Teule ya Nyerere, Emiliana Donald amekiri kupokea mwili wa askari huyo jana Alhamisi Novemba 8, 2018.

Amesema wanakusudia kufanya uchunguzi wa mwili wake wakati wowote leo Ijumaa Novemba 9, 2018 ili kuruhusu taratibu za mazishi.

Kwa mjibu wa vyanzo vya habari zinadai kuwa askari huyo mwenye cheo cha sajenti ameacha ujumbe kuwa sababu za kujiua ni kuugua tumbo muda mrefu.

Taarifa zinadai kabla ya kujiua alikuwa lindo na baada ya kufika nyumbani majira ya saa 9 alasiri aliwakuta watoto na kuwatuma soda dukani.

Baada ya kutoka alijiua kwa kujipiga risasi mbili mdomoni na kutokea kisogoni kwa kutumia bunduki aina ya SMG.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki amesema pamoja na ujumbe wa maandishi alioacha kuwa ameugua tumbo muda mrefu, alikuwa amefunguliwa jalada la kumpa mimba mwanafunzi wa sekondari.

“Kabla ya kujiua alikuwa lindo la wafungwa baada ya kufika nyumbani kwake aliwakuta watoto wake, mke hakuwepo, akawatuma kwenda kununua soda ndipo akajiua na kuacha ujumbe wa maandishi,” amesema.