In Summary

Mgombea huyo ameshindwa kura za maoni kwa kuzidiwa kwa kura moja

 


Serengeti. Diwani wa Chadema aliyejiuzulu na kujiunga CCM Michael Kunani amebwagwa katika kura za maoni ndani ya CCM, kata ya Ikoma wilaya ya Serengeti, Mara kwa kuzidiwa kura moja tu na Moses Nguhecha.

Kunani na diwani wa kata ya Manchira, Joseph Mongita walijiengua Chadema na kuhamia CCM na kuacha nafasi zao wazi, hata hivyo Mongita hakujitokeza kuchukua fomu.

Katika kura za maoni kata ya Ikoma CCM aliyeongoza ni Moses Nguhecha (18) Michael Kunani (17), Mgosi Gaugeri (1) huku wanachama watatu waliokuwa wanadaiwa kuwa na nguvu kisiasa wakiondoa majina yao.

Hata hivyo majina hayo yanasubiri baraka za kamati ya siasa wilaya na halmashauri kuu ya chama ngazi ya mkoa ili kupitisha jina la mgombea atakayepambana na vyama vingine.

Katika kata ya Manchira, Daudi Manteni alipata kura 46 na kufuatiwa na Shamina Muyuga kura 32.

Katibu wa CCM wilaya ya Serengeti, Solomoni Kasaba amesema vikao vya chini vimekamilisha michakato yake na vikao vinavyofuata vitatoa majina ya wagombea kwenye kata zote mbili.

Kwa upande wa Chadema, Katibu wa chama hicho wilaya ya Serengeti, Julius Anthony amesema wagombea watatu wamejitokeza kuchukua fomu ambao ni Eliya Wilson, Richard Nyambacha na Timani Makuru.

“Tunaendelea na mchakato wa kupata wagombea katika kata hii pamoja na Ikoma ambao utakamilika ifikapo Julai 14," amesema Anthony.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Chadema ilishinda kiti cha ubunge na kata 18 na CCM walishinda kata 12.