In Summary

Fatma Karume alishinda urais wa TLS na Ngwilimi alishika nafasi ya pili

 Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi amesema ‘uchaguzi umemalizika, tumpe ushirikiano Fatma Karume na viongozi wengine waliochaguliwa.’

Ngwilimi ameyasema hayo leo Aprili 16, 2018 kupitia waraka alioutoa akizungumzia masuala mbalimbali ikiwamo mwelekeo wake baada ya kushindwa uchaguzi huo wa TLS.

Amesema uchaguzi wa TLS uliofanyika Aprili 14, 2018 ulikuwa wa kidemokrasia na bila dosari yoyote ile hadi ukawapata ambao ni rais, makamu, wajumbe wa baraza la uongozi watakaoongoza kwa mwaka mmoja hadi 2019.

“Katika uchaguzi huo, mimi (Ngwilimi) niligombea nafasi ya urais, mwisho wa siku wakili mwenzetu Fatma Karume alichaguliwa kwa kura nyingi kuchukua nafasi hiyo kubwa na yenye heshima ya pekee si tu kwa mawakili, lakini pia katika mfumo na tasnia ya sheria na uwakili na sheria hapa nchini na kimataifa,” amesema Ngwilimi