In Summary

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezitupia lawama zilizokuwa kamati za mipango miji kuwa chanzo cha kuvurugwa miji nchini

Tabora. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezitupia lawama zilizokuwa kamati za mipango miji kuwa chanzo cha kuvurugwa miji nchini.

Akizungumza leo Ijumaa Mei 24, 2019 katika uzinduzi wa mpango kabambe wa manispaa ya Tabora, Lukuvi amesema kamati hizo  zilikuwa uchochoro wa rushwa huku madiwani wakitumia vibaya madaraka yao.

Amesema kupitia kamati hizo, madiwani kwa kushirikiana na watendaji walipora ardhi za wanyonge na kujitajirisha  kutokana na ulanguzi wa viwanja na rushwa.

Waziri Lukuvi amewataka madiwani nchini kubadilika kwa maelezo kuwa hivi sasa hakuna fursa ya kuchuma kupitia udiwani kama awamu iliyopita.

Akizungumzia Mpango Kabambe katika manispaa ya Tabora, Lukuvi amesema una manufaa mengi na mojawapo ni kuondoa migogoro ya ardhi.

“Kuzinduliwa kwa mpango huu maana yake thamani ya ardhi imepanda, mpango huu usihujumiwe,” amesema Lukuvi na kuwataka madiwani kufuufuata kama mwongozo na kutoubadilisha kwa matakwa ya utajiri au cheo.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amesema mpango huo utatoa majibu ya changamoto zilizokuwa zinaikabili manispaa ya Tabora.