In Summary

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel akiwa pamoja na  wakuu wa idara wameitikia wito wa Rais John Magufuli aliyewataka viongozi serikalini kutumia mtandao wa simu wa  Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

 

Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel akiwa pamoja na  wakuu wa idara wameitikia wito wa Rais John Magufuli aliyewataka viongozi serikalini kutumia mtandao wa simu wa  Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Leo Ijumaa Mei 24, 2019 Gabriel akiwa na wakuu hao wamekwenda katika ofisi za TTCL mkoa hapa na kununua laini ya simu za mtandao huo.

Mei 21, 2019 Rais Magufuli alitoa mwezi mmoja kwa ofisi yake na wizara mbalimbali ambazo bado hazijaanza kutumia huduma za TTCL kuanza kutumia.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo ikiwa ni muda mfupi baada ya kusomwa kwa majina ya ofisi zinazotumia mtandao wa mawasiliano wa TTCL, huku ofisi ya Rais ikiwa miongoni mwa zinazotumia mtandao huo.

Akizungumza katika hafla ya kupokea gawio la TTCL walilolitoa serikalini, Rais Magufuli amesema mbali na ofisi yake pia amesikitika kutosikia Chama cha Mapinduzi (CCM) kutumia mtandao huo licha ya kuwa katibu mkuu wake, Dk Bashiru Ally ni mzalendo.

Akizungumza katika ofisi hizo,  Gabriel amesema wameamua kumuunga mkono Rais Magufuli aliyetaka viongozi serikalini kutimia mtandao huo.

Katibu tawala wa Mkoa huo,  Denis Bandisa amesema wameamua kurudi nyumbani na kutumia mawasiliano ya TTCL  na kusisitiza kuwa kuanzia sasa halmashauri zote za Mkoa zitatumia mawasiliano ya TTCL.

Meneja wa TTCL mkoani humo,  Mohamed Shehe amesema kwa mkoa wa Geita TTCL ina wateja zaidi ya 16,000 na kuwataka Watanzania kuwaamini kwa kuwa shiriki hilo ni mali yao.