In Summary
  • Hivi karibuni mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alimwagiza katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally kuwaandikia barua wabunge wote ambao hawakuhudhuria kikao cha Bunge wakati wa upigaji kura kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali.

Dar es Salaam. Wabunge wa CCM wasiohudhuria vikao vya Bunge bila sababu za msingi kuanzia mwaka 2016 wanakabiliwa na hatua kali kutoka ndani ya chama hicho.

Hivi karibuni mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alimwagiza katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally kuwaandikia barua wabunge wote ambao hawakuhudhuria kikao cha Bunge wakati wa upigaji kura kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali.

Rais Magufuli alimtaja waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ni mbunge wa kuteuliwa kuwa hakuhudhuria kikao hicho kwa kuwa alikuwa amelazwa, lakini akipokea barua kutoka kwa Dk Bashiru atapaswa kuambatanisha na vyeti vya hospitali.

Rais aliyasema hayo Ikulu, Dar es Salaam baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni.

Akizungumzia suala hilo kwa Mwananchi juzi, Dk Bashiru alisema amekwishawaandikia barua wabunge hao, lakini uchunguzi umeanza kuanzia 2016.

Alisema kwa sasa wanafanya uchunguzi wa wabunge wa CCM ambao hawajahudhuria vikao vya Bunge kuanzia mwaka huo.

“Kama kuna watu watathibitika kutokuwapo kwenye vikao, si siku ya kupitisha bajeti tu, bali tangu mwaka 2016 watachukuliwa hatua, tutawapa taarifa. Kwa sababu bajeti ile ni chama kinaomba fedha serikalini ili kitekeleze ilani yake,” alisema. “Huo ni utaratibu wa ndani ya chama, baada ya kuwaandikia barua kuna wengine wameshajieleza, tunafanya uchambuzi wa barua zao.

“Tunakwenda mbali zaidi kwenye mahudhurio ya vikao vyote vya Bunge si hivi vya bajeti tu. Kama kuna wabunge waliokuwa na udhuru walete uthibitisho, kama kuna waliokuwa wagonjwa walete vyeti vya hospitali.”

Dk Bashiru alisema hatua hiyo inalenga kujenga nidhamu ndani ya chama hicho kwa kuwa ubunge ni mali ya chama. “Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017, nyongeza B inaeleza kuwa kuna kanuni zinazotambua kamati ya wabunge wa CCM na huko kuna utaratibu wao,” alisema mtendaji huyo mkuu wa chama hicho.

“Suala la mahudhurio ni la CCM kwa sababu ule si ubunge wao, ni wa chama. Ile ni dhamana tu wamepewa.

Dk Bashiru alisema wanafanya uchambuzi wa kina kupata ushahidi na kulinda haki za wabunge watakaotoa uthibitisho.

Wabunge ambao hawakuwepo wakati wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali ni Prosper Mbena (Morogoro Kusini), Abdulaziz Abood (Morogoro Mjini), Selemani Zedi (Bukene), Nimrod Mkono (Butiama), Lameck Airo (Rorya), Rashid Akbar (Newala Mjini), Jamal Kassim Ally (Magomeni) na Lolesia Bukwimba (Busanda).

Wengine ni Haji Ameir Haji (Makunduchi), Hassan Kaunje (Lindi Mjini), Khamis Yahya Machano (Chaani), Stephen Masele (Shinyanga Mjini), Emmanuel John (Kiteto), Hamoud Abuu Jumaa (Kibaha Vijijini), Profesa Kabudi (kuteuliwa) na Dk Augustine Mahiga (kuteuliwa).

Pia wamo Ester Mmasi (viti maalumu), Salma Kikwete (kuteuliwa), Munde Tambwe (viti maalumu) na Anne Kilango Malecela (kuteuliwa).

Alipoulizwa juzi kuhusu wabunge hao kuandikiwa barua, katibu wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza alisema baadhi hawakuwapo wakati wa upigaji kura kupitisha bajeti na si jambo la ajabu.

Rweikiza ambaye ni mbunge wa Bukoba Vijijini alisema mbunge ni binadamu na kama ilivyo kwa binadamu wengine anaweza kushindwa kuhudhuria vikao kutokana na sababu mbalimbali.

“Naomba uelewe kuwa mbunge ana jukumu la kuhudhuria vikao vya Bunge na si suala moja tu la kupiga kura, anapaswa kushiriki katika kamati, kujadili mijadala ndani ya Bunge lakini pia shughuli zozote za kibunge,” alisema.

Alizitaja sababu zinazoweza kusababisha mbunge kutohudhuria kikao kuwa ni ugonjwa, kufiwa, kuomba ruhusa kwa spika au katibu wa wabunge, kuhudhuria shughuli za kibiashara au utoro.

“Zote hizo ni dharura ambazo awe mbunge ama wa CCM au upinzani anaweza kuwa nazo, hivyo inategemea hakuweza kuhudhuria kutokana na sababu gani,” alisema Rweikiza.

Alipoulizwa iwapo walioshindwa kuhudhuria kutokana na sababu za utoro wamechukuliwa hatua, Rweikiza alisema, “hilo la barua siwezi kulizungumzia.”

Imeandikwa na Elias Msuya, Tausi Mbowe na Bakari Kiango