In Summary

Jeshi la polisi mkoani Morogoro linamshikilia Mohamed Chambo (66) mganga wa jadi na mkazi wa mji mpya manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Mkwajuni

Morogoro. Jeshi la polisi mkoani Morogoro linamshikilia Mohamed Chambo (66) mganga wa jadi na mkazi wa mji mpya manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Mkwajuni.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Mei 24, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema muhumiwa huyo alikamatwa Mei 16, 2019 maeneo ya Mji Mpya kata ya Mwembe Songo.

Amesema mwanafunzi huyo alipelekwa kwa mganga huyo na baba yake mzazi  akiwa pamoja na shangazi yake kwa ajili ya matibabu.

Kamanda huyo amebainisha kuwa mwanafunzi huyo alikuwa akisumbuliwa na kifafa na walimpeleka kwa mganga huyo tangu mwaka 2018, mganga kuwataka wazazi hao kumuacha mwanafunzi huyo kwake kwa maelezo kuwa anapaswa kulala hapo ili aweze kumhudumia vyema.

Kamanda huyo amesema mwanafunzi huyo alipohojiwa amesema alipoanza matibabu alikuwa akilala nyumbani kwa mganga huyo pamoja na wajukuu zake.

Amesema baadaye mganga huyo alianza kumfuata usiku na kumpapasa.

Mufafungwa amesema mwanafunzi huyo alibainisha kuwa alivyokuwa akipelekwa kwa ajili ya matibabu, mganga huyo alikuwa akimuingilia kimwili na kumtaka asipige kelele na akijaribu atamgeuza msukule.

“Kila ilipofika majira ya usiku nilihisi napapaswa  na nilipofungua macho nilimuona babu anafanya kitendo hicho alinikataza nisipige kelele kwani nikifanya hivyo atanifanya kuwa msukule na nikaogopa,” amesema Mutafungwa akinukuu maelezo ya mwanafunzi huyo.

Kamanda huyo wa Polisi amebainisha kuwa mganga aligeuza kitendo hicho kuwa mchezo wa karibu kila siku.

Amesema Mei 16, 2019 mwanafunzi huyo alienda  kwa mtuhumiwa huyo na  kufanya naye mapenzi kama ilivyo kawaida yao.

Mutafungwa amesema mmoja wa wanafunzi wenzake alimuona akingia nyumbani kwa mganga huyo na alivyotoka akamuuliza alikwenda kufanya nini, ndipo alipoeleza alichokwenda kufanya.

Amesema rafiki wa mwanafunzi aliyekuwa akifanyiwa udhalilishaji  alitoa taarifa kwa mmoja wa walimu wao na uongozi wa shule kumuita shangazi yake na kumpa taarifa hizo.

 

Amesema mganga huyo anashikiliwa na atafikishwa mahakamani uchunguzi ukikamilika.