In Summary

Marwa anayefanya biashara ya kukusanya na kuuza vyuma chakavu katika mikoa ya Mara na Mwanza, amesema alishtuka kuona kitu kisicho cha kawaida wakati vijana wake walipokuwa wakipakia vyuma chakavu kwenye gari tayari kusafisrishwa kwenda jijini Mwanza.

Serengeti. Bomu lenye uzito wa kilo 10 limegundulika ndani ya vyuma chakavu vilivyokuwa vikiandaliwa kusafirishwa kutoka mjini Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwenda jijini Mwanza. 

Bomu hilo limegunduliwa na mfanyabiashara wa vyuma chakavu, Jonas Marwa leo Ijumaa Mei 23, 2019, limeharibiwa na Wataalamu wa mabomu kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) katika eneo la Borenga wilayani Serengeti. Eneo hilo linatumiwa kwa shughuli za kijeshi.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mara waliotembelea wilaya ya Serengeti leo Mei 24, 2019, Meja Patrick Kitosi kutoka Kikosi cha Jeshi cha 27 amesema bomu hilo linawezekana ni masalia ya mabomu yaliyoharibiwa mwaka 2000.

“Wananchi wanapoona vitu wasivyovijua kwenye maeneo yao watoe taarifa polisi au kwenye mamlaka yoyote ya Serikali ili kuepusha madhara,” amesema Meja Kitosi

Akielezea alivyolibaini bomu hilo, Marwa anayefanya biashara ya kukusanya na kuuza vyuma chakavu katika mikoa ya Mara na Mwanza amesema alishtuka kuona kitu kisicho cha kawaida wakati vijana wake walipokuwa wakipakia vyuma chakavu kwenye gari tayari kusafirishwa kwenda jijini Mwanza.

“Baada ya kulitilia shaka kitu hicho, nilitoa taarifa polisi ambao walifika wakiwa na mshauri wa mgambo na kubaini kuwa ni bomo na kuondoka nayo,” amesema Marwa

Amesema anaendelea kufuatilia kutoka kwa vijana wake wanaomsaidia kukusanya vyuma chakavu kutoka kwa wananchi kama wanamkumbuka aliyewauzia bomu hilo ili kusaidia vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi iwapo bado anavyo vingine.