In Summary

Viongozi wa watani wa jadi, Simba na Yanga kwa nyakati tofauti leo wamezungumzia tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ na kuwataka mashabiki wa soka kuwa na subira na kuungana kuhakikisha anapatikana salama


Dar e Salaam. Uongozi wa klabu ya Simba umewaomba mashabiki na wanachama wake kuwa watulivu  wakati Jeshi la Polisi likiendelea kumtafuta mwekezaji wa timu hiyo, Bilione Mohammed Dewji “Mo Dewji” ambaye ametekwa leo alfajili.

Wito huo umetolewa baada ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kukumbwa na taharuki kuhusiana na tukio la kutekwaji bilionea huyo ambaye mpaka sasa ameifanyia mambo makubwa klabu ya Simba.

Msemaji wa klabu ya Simba, Hajji Manara alisema Jeshi la Polisi lipo katika harakati za kuhakikisha Mo Dewji anakuwa salama na kuwakamata watekaji.

“Naomba tuwe na subira kwani Jeshi  la Polisi linafanya kazi yake, naomba hata familia iwe na subira katika sakata hili, tuwaache polisi kufanya kazi yake na tusubiri majibu. Hata mkuu wa mkoa naye yupo katika harakati za kuhakikisha MO anarejea na kuendelea na shughuli zake,” alisema Manara.

Soma zaidi:

 

 

 

 

 

Alisema anajua taarifa za kutekwa kwa MO Dewji zimewastua wapenzi wa Simba na wadau  wa sekta zote kutokana na shughuli za mwekezaji huyo.

Aliwataka wana Simba wawe watulivu na kuliachia Jeshi  la Polisi kufanya kazi yake na kwamba wana amini MO atapatikana akiwa hai.

Wakati huo huo: Uongozi wa klabu ya Yanga umewataka mashabiki wake kuungana na wale wa Simba kumuombea MO apatikane akiwa salama.

Msemaji wa Yanga, Dismas Ten amesema wamesikitishwa na utekwaji wa MO ambaye amesaidia kuleta maendeleo ya soka nchini, hasa kwa watani wao wa jadi.

“Sijisikii vizuri, nimeamka na kukutana na suala hili la kusikitisha, nawaomba mashabiki na wanachama wa Yanga kuungana na watani zetu ili MO apatikane salama na kuungana na familia yake na ya    wanamichezo kwa ujumla,” amesema Ten.