In Summary

Mwakyembe amewataka wasanii hao kuandaa filamu bora na kuacha kuiga za nje ili waweze kuliteka soko la kimataifa

Babati. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wasanii wa filamu nchini kuandaa filamu bora zaidi kwani Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa kutengeneza filamu nyingi ikitanguliwa na Nigeria.

Dk Mwakyembe ameyasema hayo leo Julai 11 akiwa Babati, Manyara kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wasanii 951 wa mikoa tofauti.

Amesema wasanii wakibadilika na kuacha kuiga matendo, mandhari, mavazi na utamaduni wa filamu za nje wataweza kuteka soko la kimataifa la filamu kwani Watanzania wanatengeneza filamu nyingi mno.

"Mfano hapa Manyara kuna mbuga za wanyama, kuna makabila ya wamasai, wairaqw na wadatoga mnaweza kubadili mazingira kwani magorofa na suti watu wameshazoea kuona wanataka vitu vipya," amesema Dk Mwakyembe.

Amesema wasanii nchini hata wakiwatumia waganga wa kienyeji hawataweza kupiga hatua endapo wasipobadilika kwa kuandaa miswada bora na kuzingatia uhalisia.

Katibu Mtendaji wa bodi ya filamu Tanzania, Joyce Fissoo, amesema wasanii wa wilaya ya Hanang mkoani Manyara wameshawahi kushinda tuzo ya filamu ya kimataifa.