In Summary

 Jana alitangaza kuachana na siasa na hapo hapo akatangaza kurejea CCM

Kahama. Huenda mwanasiasa mkongwe nchini, James Lembeli ameutumia usemi usemao, ‘hakuna kama mama’.

Katika tukio la aina yake, Lembeli ambaye amewahi kuwa mbunge wa Kahama, jana alitangaza kuachana na siasa na hapo hapo akatangaza kurejea CCM, baada ya mama yake kusimama mbele ya umati wa watu na kumshawishi arejee katika chama hicho tawala.

Lembeli alihamia Chadema 2015 na kugombea ubunge wa Jimbo la Kahama akichuana na Jumanne Kishimba (CCM). Alishindwa katika uchaguzi huo.

Awali, jana akizungumza na wanahabari nyumbani kwake, Kijiji cha Mseki, Ushetu alieleza kuwa ameachana na siasa kwa kuwa amebanwa na taratibu za taasisi na mashirika ya kimataifa anayofanya nayo kazi.

Pia alisema kuwa amekosana na familia yake ikiwamo ya wana CCM walioacha kufanya maombi kwenye kaburi la baba yake aliyekuwa mtemi baada ya kuhamia Chadema.

“Hapa kwetu kuna kaburi la mtemi baba yangu. Siku hizi watu wa CCM hawaji kuomba dua kwenye kaburi hivyo nimeamua nisiwe na chama ili watu waendelee kuomba,” alisema.

“Napumzika siasa ila mimi bado mchezaji mzuri naamini kila chama nitakachoenda namba yangu ipo tu.”

Baada ya kueleza hayo, ndugu na wanahabari walimuhoji iwapo atahamia chama kingine na ni kipi.

Akiwa bado ameshikilia msimamo wa kutotangaza chama, mama yake mzazi, Maria Lembeli (80), alinyanyuka na kumtaka kutangaza mara moja kurejea CCM akieleza kitendo chake cha kuhamia Chadema kilimsononesha yeye na familia.

“Kitendo chako cha kuhama CCM kilinisononesha sana kwa sababu marehemu baba yako (Daudi Lembeli) alikuwa mwana CCM hadi kufa kwake. Nilikuruhusu kuhamia Chadema shingo upande na tangu wakati huo nimeishi na maumivu moyoni,” alisema Maria akimsihi mtoto wake kurejea CCM.

Mbali ya mama, shinikizo jingine pia lilitoka kwa kaka yake, Peter Lembeli aliyemtaka kurejea CCM ili kurejesha haiba ya familia iliyopotea.

Akionekana kuelemewa na shinikizo na kauli za mama na kaka yake, Lembeli alisimama na kutangaza kurejea CCM akidai ni njia ya kumheshimu mama yake ambaye hakujua kama aliumia yeye kuhamia upinzani.

“Sikujua kama uamuzi wangu wa kuhama CCM ulimuumiza kiasi hicho mama yangu; natangaza kurejea CCM ili mama yangu awe na amani. Nawaomba radhi wote niliowakwaza kwa uamuzi wangu wa kuhamia Chadema,” alisema Lembeli.

Kiongozi pekee wa CCM aliyehudhuria tukio hilo, Paulina Ndutu alisema kurejea CCM kwa Lembeli kumemrejeshea furaha kutokana na wakati mgumu aliokuwa akipata wa kushirikiana naye kutokana na urafiki wao wa tangu akiwa chama tawala.