In Summary

Katika michuano ya mwaka huu, Afrika inawakilishwa na Senegal, Nigeria, Tunisia, Morocco na Misri, lakini nchi zote tano zikionekana kutokuwa na makali ya kutosha.

Misri


Moscow, Russia. WAKATI michuano ya Kombe la Dunia ikitarajiwa kuanza kutimua vumbi leo, swali kubwa linalogonga vichwa vya mashabiki na Waafrika wote kwa ujumla ni nchi gani inayoweza kututoa kimasomaso kwa angalau kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Katika michuano ya mwaka huu, Afrika inawakilishwa na Senegal, Nigeria, Tunisia, Morocco na Misri, lakini nchi zote tano zikionekana kutokuwa na makali ya kutosha.

Misri

Misri maarufu kama ‘Pharaoh’ iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vyema inaonekana kunyong’onyea baada ya kuumia mshambuliaji wake mahiri Mohamed Salah ‘Mo’.

Mshambuliaji huyo aliyekua kwenye kiwango cha juu msimu huu, aliumizwa bega na beki wa Real Madrid, Sergio Ramos, katika mchezo wa fainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Madaktari wanapambana kwa kila hali kuhakikisha mshambuliaji huyo anapona na kuisaidia nchi yake kuanzia katika mechi ya pili ya hatua ya makundi.

Kuumia kwa Salah ni pigo sio tu kwa Misri ni Afrika nzima kutokana na ukweli kwamba kiwango chake kiliwafanya wengi kuamini kuwa atafanya mambo makubwa kwenye fainali za mwaka huu.

Misri imepangwa Kundi A na wenyeji Russia, Saudi Arabia na Uruguay. Mechi ya kwanza itacheza kesho dhidi ya Uruguay mjini Ekaterinburg.

Kwa kuwa ina washambuliaji wawili pekee kwenye kikosi hicho, katika mchezo wa kesho kocha Hector Cuper, hatakuwa na chaguo jingine zaidi ya kumpanga mchezaji asiyekuwa na uzoefu Marwan Mohsen wa Al Ahly kuongoza mashambulizi.

Kukosekana kwa Salah kunaifanya Misri isiwe tena tegemeo zaidi la Waafrika, badala yake wengi wanabaki wakijiuliza ni Senegal, Nigeria, Tunisia au Morocco itakayowabeba?.

Senegal ‘Simba wa Teranga’ inayonolewa na Aliou Cisse, inashika nafasi ya 27 kwa ubora wa soka duniani, licha ya kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, lakini matumaini ya wengi yapo kwa mshambuliaji mahiri wa Liverpool, Sadio Mane, aliyeng’ara msimu huu.

Senegal ipo Kundi H na Poland, Colombia, Japan na kikosi chao kinaundwa na nyota wote wanaocheza soka Ulaya, makipa wakiwa; Abdoulaye Diallo, Alfred Gomis na Khadim Ndiaye. mabeki ni; Lamine Gassama, Saliou Ciss, Kalidou Koulibaly, Kara Mbodii, Youssouf Sabaly, Salif Sane na Moussa Wague.

Viungo Idrissa Gueye, Cheikhou Kouyate, Alfred Ndiaye, Badou Ndiaye, Cheikh Ndoye na Ismaila Sarr. Washambuliaji Keita Balde, Mame Biram Diouf, Moussa Konate, Mbaye Niang, Diafra Sakho, Moussa Sow na Mane.

Morocco ‘Simba wa Atlas’

Mafanikio ya soka kwa kocha Herve Renard hasa katika mechi za fainali yanatia matumaini kwamba pengine Morocco inaweza kufika mbali kwenye michuano hiyo.

Morocco inayoshika nafasi ya 41 kwa ubora duniani, imepangwa Kundi B na Iran, Hispania, Ureno.

Kikosi kinaundwa na makipa; Monir El Kajoui, Yassine Bounou na Ahmed Reda Tagnaouti. Mabeki Nabil Dirar, Marouane Da Costa, Ghanem Saiss, Hamza Mendyl, Medhi Benatia, Achraf Hakimi na Sofiane Amrabat.

Viungo Karim Al Ahmadi, Youssef Ait Bennasser, M’bark Boussoufa, Faycal Fajr, Amine Harit, Noureddine Amrabat, Hakim Ziyach na Younes Belhanda.

Washambuliaji Ayoub Al Kaabi, Khalid Boutaib, Aziz Bouhaddouz, Mehdi Carcela Gonzalez na Youssef En-Nesyri.

Tunisia

Vijana hawa wa kocha Nabil Maaloul, wanashika nafasi ya 64 kwa ubora wa soka duniani na wamepangwa Kundi G na England, Panama, Ubelgiji ambapo wataanza kurusha karata ya kwanza Jumatatu kwa kuikabili England.

Kikosi chao kamili kinaundwa na makipa; Farouk Ben Mustapha, Moez Hassen na Aymen Mathlouthi. Mabeki Rami Bedoui, Yohan Benalouane, Syam Ben Youssef, Dylan Bronn, Oussama Haddadi, Ali Maaloul, Yassine Meriah na Hamdi Nagguez.

Viungo Anice Badri, Mohamed Amine Ben Amor, Ghaylene Chaalali, Ahmed Khalil, Saifeddine Khaoui, Ferjani Sassi, Ellyes Skhiri, Naim Sliti na Bassem Srarfi. Washambuliaji Fakhreddine Ben Youssef, Saber Khalifa na Wahbi Khazri.

Nigeria ‘Super Eagles’

Hawa wapo Kundi D na Iceland, Croatia, Argentina, wanashika nafasi ya 48 kwa ubora wa viwango duniani, wananolewa na kocha Gernot Rohr, wachezaji nyota aki wemo nahodha John Obi Mikel, Victor Moses na Ahmed Musa.

Kikosi kinajumuisha makipa; Ikechukwu Ezenwa, Francis Uzoho na Daniel Akpeyi. Mabeki Abdullahi Shehu, Tyronne Ebuehi, Elderson Echiejile, Bryan Idowu, Chidozie Awaziem, William Ekong, Leon Balogun na Kenneth Omeruo.

Viungo John Obi Mikel, Ogenyi Onazi, Wilfred Ndidi, Oghenekaro Etebo, John Ogu na Joel Obi wakati. Washambuliaji Ahmed Musa, Kelechi Iheanacho, Victor Moses, Odion Ighalo, Alex Iwobi na Simeon Nwankwo.

Kuffour alonga

Aliyekuwa beki mahiri wa zamani wa Ghana ‘Black Stars’ ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, Samuel Osei-Kuffour, anasema hana matumaini kuona timu za Afrika zinafanya maajabu na kutinga nusu fainali, katika fainali za Kombe la Dunia 2018.

Kuffour anasema katika michuano hiyo inayoanza leo, timu za Afrika hazijaonyesha maandalizi ya kutosha na hazina hamasa ya kutosha ya kuzisukuma kufanya makubwa.

“Licha ya kushiriki katika kila fainali Afrika imefika hatua na robo fainali mara tatu pekee mwaka 1990 Cameroon, 2002 Senegal na 2010 Ghana, rekodi inatuthibitishia kuwa hatuna miujiza ya kufanya,” anasema Kuffour.