In Summary

Lopetegui ametimuliwa kuinoa Hispania kabla ya kuanza fainali za Kombe la Dunia nchini Russia 

Moscow, Russia.Kocha mpya wa Hispania Fernando Hierro, amesema wachezaji wa Hispania hawapaswi kuomboleza baada ya kutimuliwa kocha wao Julen Lopetegui.

Lopetegui ametimuliwa kuinoa Hispania moja kabla ya kuanza fainali za Kombe la Dunia nchini Russia na kuibua mjadala mzito.

Kocha huyo alipoteza kazi baada ya Real Madri kumtangaza ndiye mrithi wa Zinedine Zidane aliyejiuzulu hivi karibuni.

Chama cha Soka Hispania, kilichukizwa na kitendo cha Lopetegui kuingia mkataba na Real Madrid kinyemela wakati akiwa na majukumu ya kitaifa.

Hierro, nahodha wa zamani wa Hispania, alisema wachezaji wanatakiwa kusonga mbele kwa kujikita katika fainali hizo.

Alisema ana amini wachezaji wote wako upande wake na wanamuunga mkono katika kampeni ya kuwania ubingwa wa dunia katika fainali hizo.

Hiero, aliyekuwa beki mahiri wa kati, alisema hali ndani ya kambi ni shwari na ana matumaini ya kufanya vyema katika michuano hiyo.

Kocha huyo mwenye miaka 50, amemtakia kila la kheri Lopetegui katika kazi yake mpya Real Madrid. Hispania leo inakata utepe kwa kuvaana na Ureno.