In Summary

Gharama kubwa zimetumika kwa ulinzi wa viongozi hao wakiwemo mabodigadi 12 wa Kim waliokimbia kando ya gari la kiongozi wao kutoka uwanja wa ndege.

Singapore. Gharama za mkutano wa kilele kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi mkuu wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un ulipangwa kugharimu dola za Marekani 20 milioni (Sh 45 bilioni), alisema Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumapili Lee alisema, “Ni gharama ambazo tuko radhi kulipa.” Lee aliongeza huo ni mchango wao katika masuala ya kimataifa na kwamba yote ni kwa “maslahi makubwa” ya Singapore.

Lee hakufafanua maslahi hayo lakini Bodi ya Utalii ya Singapore (STB) imesema kwa upande wake ilitarajia kukusanya dola 21 milioni kutokana na watalii 4,000 ambao wanatarajiwa kuingia katika kipindi hiki.

Makadirio ya STB ni kwamba watalii hao wanaweza kukaa wastani wa siku 3.5.

Masoko ya ubadilishaji fedha nayo kipindi hiki yanatarajia kupata wageni wa kutosha watakaobadilisha sarafu.

Mchanganuo

Waziri mkuu huyo alisema nusu ya fedha hizo zilipangwa kutumika kwa ajili ya masuala ya usalama ikijumuisha walinzi 12 wa Kim Jong-un waliokuwa wakikimbia kando ya gari lake kutoka uwanja wa ndege hadi kwenye eneo la mkutano.

Lee alieleza kwamba kutokana na mazingira ya mkutano huo kuhusisha maofisa wa ngazi ya juu, mahitaji ya usalama pia yalikuwa makubwa kuliko matukio mengine yote ya kisiasa.

Mbali ya uwepo wa idadi kubwa ya maofisa wa polisi, maofisa usalama walihusika “kulinda maeneo yote na kwa kina – ulinzi wa nga, baharini na ardhini – dhidi ya uwezekano wa shambulio lolote au tukio lolote la bahati mbaya.”

Gazeti la Kiingereza la Straits Times la Singapore lilinukuu chanzo kutoka Wizara ya Habari na Mawasiliano ikisema kiasi cha dola 5 milioni (Sh 11.376 bilioni) zilitumika kwa ajili ya kituo kwa wanahabari katika jengo la F1 Pit Building.

Kiasi kilichosalia kilipangwa kutumika kwa ajili ya malazi ya wanahabari wapatao 2500 kutoka pande mbalimbali za dunia na pia maofisa waliokuwa katika msafara wa Trump na Kim.

Viongozi wawili hao – Trump akitokea katika taifa kubwa kiuchumi na demokrasia na Kim akitokea taifa lisilo na maendeleo makubwa – waliwasili Singapore Jumapili, walikutana ana kwa ana kabla ya kuwa pamoja na washauri wao kisha wakapata chakula cha pamoja.

Mwaliko

Katika mkutano huo Trump alimwalika Kim kutembelea Marekani na Kim alimpa pia mwaliko Trump. Kim amekubali kuitembelea Marekani.